KMC, Mbao ngoma bado ngumu

Muktasari:

Mchezo huo wa Ligi Kuu unapigwa katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza,ambapo hadi sasa ni mapumziko na hakuna timu iliyoona lango la mwenzake.

LICHA ya kwenda mapumziko kwa nguvu sawa ya bila kufungana, KMC itajilaumu kutokana na kushindwa kutumia vyema nafasi walizopata huku kipa wa Mbao, Abdallah Makangana akifanya kazi ya ziada kwa kuokoa hatari nyingi.

Mchezo huo ambao unapigwa Uwanja wa CCM Kirumba jijini hapa, ulianza saa 10:30 jioni kutokana na shughuli zilizokuwa zinaendelea za maandalizi ya sherehe za maadhimisho ya Uhuru ambayo kitaifa yatafanyika kwenye uwanja huo.

Timu hizo zilishuka uwanjani zikiwa na kumbukumbu ya kupoteza mechi zilizopita, licha ya pande zote kuonyesha ushindani lakini KMC walionekana kuwazidi wapinzani kutokana na walivyoumudu mchezo kwa dakika 45.

Katika mechi zilizopita, KMC ilipokea kisago cha mabao 2-1 dhidi ya Alliance katika dimba la Nyamagana huku Mbao wakiloa bao 1-0 mbele ya Azam mpambano uliopigwa CCM Kirumba.

KMC walitengeneza mashambulizi mengi lakini straika wao Salim Aiyee alishindwa kuonyesha ubora kufuatia hatari zake kuokolewa na Makangana huku mashuti mengine yakitoka nje ya lango.

Hata hivyo, Mbao walijaribu kujitutumua kwa mashambulizi ya kushtukiza lakini mashuti mengi yalitoka nje ya lango na mengine kuishia mikononi mwa kipa Jonathan Nahimana.