Job achekelea kukutana na Kapombe

BEKI chipukizi wa Mtibwa Sugar,  Dickson Job amefurahia kujumuishwa kwenye kikosi cha Taifa Stars,  kilicho chini ya kocha Etienne Ndayiragije, kwamba inamsaidia kumjenga kuwa na uzoefu wa kucheza michuano mbalimbali ya kimataifa.

Amesema kitendo cha kocha Ndayiragije kumuona anaweza kuwa na mchango ndani ya kikosi hicho, kimempa moyo wa kupambana akiamini kazi zake zinaonekana mbele ya Watanzania, hivyo anaona deni limebakia kwake.

"Nimejisikia faraja kuona kumbe kocha ameona nina kitu, kwani nafasi yangu ya beki tupo wengi ligi kuu, lakini kuchaguliwa mimi kunanifanya nijibidishe zaidi ili nisimuangushe katika lengo lake,"amesema Job na amengeza kuwa.

"Hakuna mchezaji ambaye hapendi kuchezea timu yake ya taifa, ndio maana hata hao wa kigeni TFF ilishatangaza kwamba kwenye mataifa yao wawe wanachezea timu zao za taifa, kiukweli nina furaha sana kuwa miongoni mwa walioaminiwa kuunda kikosi kitakachoikabili Burundi,"amesema.

Amesema alizoea kucheza timu za taifa za vijana na ndoto zake zilikuwa nikucheza yawakubwa, hivyo anajiona amepiga hatua kubwa na anatamani kufanya makubwa ya kuacha alama kama ilivyo kwa wachezaji ambao wanategemewa kama Shomary Kapombe.

"Kuchanganyika na wachezaji wenye uzoefu na wanaoaminiwa kwenye kikosi cha Stars kama Kapombe, kunanipa nafasi yakujifunza vitu vingi kutoka kwao, hivyo naamini sitaondoka bure baada ya majukumu yaliopo mbele yetu,"amesema.