JB, Mzambia wakoleza moto

Juma Balinya ‘JB’

MASHABIKI wa Yanga waliopo mjini Morogoro wanahesabu saa tu kabla ya kuanza kupata utamu kutoka kwa nyota wa timu hiyo ilisafiri hadi mkoani humo ili kuanza kambi leo Jumatatu, huku Mzambia Maybin Kalengo akikoleza moto kwa mashabiki hao.

Mashabiki wa Yanga mjini humo wamesisitiza wanahamu ya kutaka kuona kikosi kipya, lakini wangependa kumuona Mzambia Kalengo ambaye wamekuwa wakisikia sifa zake za kucheka na nyavu tangu akiwa Zesco United inayonolewa na Kocha George Lwandamina.

Mapro wote wa kigeni wameshawasili nchini isipokuwa Sadney Urikhob inayeelezwa ana matatizo ya kifamilia kwao, Namibia na anatatua kesho Jumanne sambamba na winga, Deus Kaseke aliyetoka kuoa wikiendi iliyopita jijini Mbeya.

Jeshi zima lililosalia la Yanga tayari lipo mjini Morogoro, huku ikifichuliwa siri za kuwekwa kwa kambi hiyo mjini Morogoro kwa msimu wa tatu mfululizo.

Kambi hiyo ya Yanga ni maalumu kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara na michuano ya kimataifa na mabosi wa Jangwani wamepanga kuwatambulisha nyota wao wa kikosi cha msimu ujao kwenye Tamasha lao Maalumu la Siku ya Mwananchi.

Tamasha hilo litafanyika Agosti 3 badala ya Julai 27 jijini Dar es Salaam, ikiambatana na mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya klabu kutoka nje ya nchi.

Mnamibia, Urikhob na wazawa Kelvin Yondani na Feisal Salum ‘Fei Toto’ waliokuwa kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars ndio pekee ambao walikuwa na wasiwasi wa kushindwa kuianza mapema kambi hiyo inayoanza leo, ila Mnambia atatua kesho.

Yondani na Feisal wameshindwa kwenda Morogoro baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuomba kupunguziwa gharama ya kuwarudisha Dar kujaindaa na maandalizi ya Stars kwa mechi ya kuwania fainali za Chan 2020.

Ukiacha wachezaji hao, nyota wengine wote wa Yanga walio kwenye usajili wa msimu ujao kama Klaus Kindoki, Papy Tshishimbi, Mohamed Issa ‘Banka’, Mrisho Ngassa, Rafael Daud, Ali Ali, Ally Mtoni, Lamine Moro, Seleman Mustapha, Abdulaziz Makame, Patrick Sibomana, Mapinduzi Balama na straika matata na Juma Balinya ‘JB’ wameshatua Moro.

Ikiwa kambini hapo, Yanga itajifua chini ya Kocha Msaidizi, Noel Mwandila akisaidiana na Peter Manyika anayechukua nafasi ya Juma Pondamali, kwa vile Kocha Mkuu, Mwinyi Zahera yupo Misri na kikosi cha DR Congo ambacho usiku wa jana Jumapili kilikuwa kikicheza na Madagascar kwenye mechi ya 16 Bora ya Fainali za Afcon 2019.

Kutoka Morogoro inaelezwa mashabiki wamekuwa na kiu ya kukiona kikosi hicho, huku nyota wa kigeni akiwamo Kalengo, JB na Makame wamekuwa hawaishi kutajwa mdomoni.

SIRI YA KAMBI

Kambi ya mjini Morogoro imekuwa kama ya kudumu kwa Yanga, lakini imebainika sababu ya klabu hiyo kukimbilia mjini humo.

Chanzo kutoka Yanga kinasema Yanga imekuwa inakimbilia Morogoro kwa vile kigogo na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa klabu hiyo, Hamad Islam kukubali kubeba jukumu la kuipangia timu hiyo hoteli itakayokaa muda wote watakapokuwa mjini hapo.

Mwanaspoti imedokezwa, Islam amewapa hoteli yake ya mjini hapo kwa lengo la kuhakikisha timu hiyo inajiandaa ikiwa katika mazingira mazuri.

“Kambi ya Morogoro imegharamiwa na kiongozi mmoja wa mjini hapo ambaye ametoa hoteli yake kwa ajili ya wachezaji hao kujihifadhi hadi hapo watakapokuwa wamekamilisha maandalizi yao,” kilisema chanzo hicho.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela, alikiri wamekuwa na utamaduni wa kuomba wanachama wao kuichangia klabu yao, hivyo kuwepo kwa suala la kufadhiliwa na mjumbe huyo sio ajabu kwao.