Jamani! kumbe ishu ya Sancho ipo hivi?

DORTMUND UJERUMANI. HABARI ndo hivyo. Kinachosemwa ni kwamba winga wa Borussia Dortmund, Jadon Sancho amedaiwa kuwa na dalili zote za kusaini kuichezea Manchester United wakati dirisha la usajili wa majira ya kiangazi litakapofunguliwa.

Licha ya kuwapo na mtikisiko wa uchumi uliosababishwa na janga la corona, Man United bado imeonekana kuwa vizuri kimtindo kwenye mambo ya mkwanja na kuwa na uwezo wa kutumia Pauni 100 milioni kusajili mchezaji mmoja.

Ripoti za awali zilidai kwamba Man United waliona haitaleta maana kulipa pesa nyingi hivyo kumsajili mchezaji mmoja katika mazingira kama haya ambayo kila mtu analia ukata uliosababishwa na janga la virusi vya corona duniani kote.

Hata hivyo, kwa mujibu wa David Ornstein, winga huyo wa kimataifa wa England bado uhamisho wake upo palepale kwamba, anatarajiwa atakwenda kujiunga na miamba hiyo ya Old Trafford baadaye mwaka huu.

Akizungumza, Ornstein alisema: “Sancho anatarajia kuhama kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi na kuna nafasi kubwa ya jambo hilo kutokea.

“Kuna makubaliano baina ya Sancho na Borussia Dortmund kwamba, kama kutakuwa na ofa nzuri mezani, basi hakutakuwa na mjadala zaidi ya kumwaachia aondoke na hakuna kipingamizi chochote ambacho kitafanya Dortmund wapingane na makubaliano hayo.

“Wapo tayari kufanya kile kilichokubaliwa. Lakini, wanachohitaji wao ni ada isiyopungua Pauni 107.65 milioni au Pauni 116.63 milioni, kama kiwango walichopokea wakati walipompiga bei Ousmane Dembele.”

Na kutokana na Sancho kubakiza miaka miwili tu kwenye mkataba wake wa sasa, Man United wanaamini watampata Sancho kwa bei ya chini zaidi kwa sababu kama Dortmund watagoma na mchezaji mwenyewe akigoma kusaini dili jipya basi watakuwa kwenye hasara ya kumuuuza kwa bei ya chini zaidi katika dirisha la majira ya kiangazi mwakani. Hapo ni Manchester United wenyewe tu.