Idi Pazi : Shilingi ndo ilitunyima kucheza Afcon Ghana

Muktasari:

  • Idi Pazi anasema, mechi ya mwisho baina ya Stars na Uganda ndiyo ilikuwa inaamua nani afuzu, dakika 90 zikaisha timu hizo zikiwa sare ya bila kufungana.

KATIKA mwendelezo wa makala za nyota walioitikisa kwenye fainali za Afrika (Afcon), wakiwa na kikosi cha Stars, leo tunamleta kwako kipa namba moja wa Simba, Idi Pazi ambaye anaeleza namna Stars ilivyokosa nafasi ya kushiriki Afcon baada ya kufanyika uamuzi wa kurusha Shilingi.

Idi Pazi, ambaye anamini kama sio uamuzi huo, Taifa Stars ingekuwa na historia ya kushiriki fainali hizo mara mbili, nafasi inayotafutwa sasa kama Stars itaipata basi ingekuwa ni ya tatu kwa Tanzania kushiriki fainali hizo za mataifa ya Afrika.

Safari ya kwanza ya Stars Afcon ilikuwa hivi. Kipa huyo anakumbuka namna Stars ilivyotolewa na Uganda mwaka 1977 ikiwa imebakiza hatua chache kufuzu, lakini uamuzi wa kurusha shilingi na kuchagua kati ya kichwa au Mwenge ndiyo uliwaponza na Stars kutolewa mashindanoni.

“Wakati ule hakukuwa na utaratibu wa kupiga penati, mechi yetu ya mwisho ya kufuzu Afcon iliamuliwa na matokeo ya shilingi,” anasimulia Idi Pazi.

Anasema kwenye kundi lao, walikuwa na timu ya Misri na Uganda, wakati ule hakukuwa na mechi ya ugenini wala nyumbani, timu zote zilikwenda kwenye kituo cha mashindano.

“Kwenye kundi letu, Misri ndiyo walikuwa wenyeji, timu mbili ndizo zilipaswa kufuzu kucheza Afcon, nakumbuka hatukuwa na maandalizi ya kina, tulijikusanya wiki moja tukafanya mazoezi kabla ya kwenda Misri kwenye zile fainali.

“Mechi ya kwanza tulifungwa na Misri 2-1, Uganda nao wakafungwa 2-0, hivyo Misri akawa amefuzu, ikabaki sisi na Uganda, timu ipi itakayoungana na Misri kwenye fainali za 1978 zilifanyika Ghana,” anasimulia.

Idi Pazi anasema, mechi ya mwisho baina ya Stars na Uganda ndiyo ilikuwa inaamua nani afuzu, dakika 90 zikaisha timu hizo zikiwa sare ya bila kufungana.

“Wakati ule hakukuwa na sheria ya penati wala kuongeza muda, refarii alikuwa anakuja na shilingi na bingwa anapatikana kwa stahili hiyo.

“Nahodha wetu, Jella Mtagwa alikwenda kuchagua upande wa shilingi, alichagua Mwenge na Uganda wakachagua kichwa, wachezaji wote tulikuwa tumekaa tunazama lile tukio.

“Refarii akarusha Shilingi, basi Uganda wakatoka wana furahi sababu Shilingi iliwapelela Afcon ya 1978 na sisi safari yetu ikawa imeishia pale.

Anasema, licha ya kutolewa kwa shilingi, lakini matokeo yale wala hayakuwasumbua, kwani kwa mpira wa uwanjani, walikuwa fiti kweli kweli hivyo wakarudi kujipanga upya wakiwa chini ya makocha wazawa, Joel Bendera (Marehemu) na Rey Gama.

VITA YA KAGERA ILIWAWEKA KANDO NA MPIRA

Idi Pazi anasema baada ya kurejea nchini, kila kitu kilivurugika, hawakujipanga kama ambavyo walipanga mwaka 1978, kwani nchi ndiyo ilikuwa imeingia kwenye vita ya kumng’oa nduli Idi Amin, hivyo masuala mengi yalisimama wakati huo.

“Hata mambo ya mpira kidogo yalisimama, hatukuendelea na maandalizi kwa ajili ya Afcon iliyofuata kama tulivyopanga mwaka 1978, hadi mwaka 1979 ndipo tukaanza kujiandaa na ile ya 1980 iliyofanyika Nigeria.

“Mwaka huo tulikuwa na maandalizi mazuri sana, tulianza kucheza na timu ya Taifa ya Malawi, tulicheza mechi tatu za kirafiki na timu ile ambazo zilifanyika mikoa tofauti nchini humo, tuliporejea nchini tukaenda Madagascar ambako tulicheza mechi mbili na timu ya kule ndipo tukaanza harakati za kufuzu,” anasema.

Anasema kikosi kilichocheza mwaka 1977 hakikubadirishwa sana, waliongezwa wachache tu kwani Stars ya wakati ule ilikuwa ikijielewa uwanjani na walijua kucheza mpira.

“Kwenye mnechi za kufuzu 1979 mambo yalibadirika hapa tulikuwa na mechi za nyumbani na ugenini, mechi ya kwanza ya kufuzu tulicheza na Maurtius ambapo tulianzia ugenini tukafungwa 3-2, nyumbani tuliwafunga 4-0, tukacheza na Madagascar mechi ya pili ambapo nyumbani tuliwafunga 2-0, ugenini tukatoka sare ya 1-1, kisha tukacheza na Zambia ambapo nyumbani tulishinda 1-0 na ugenini tukatoka 1-1.

Nini Tino, kuna mtu anaitwa Omary Hussein

Bila shaka ukizungumzia nafasi ya Stars Afcon, wengi watalitaja bao la Peter Tino nyota wa zamani wa Yanga kuwa ndilo lililoipa nafasi Stars kucheza Afcon ya 1980.

“Achana na Tino, Stars ya wakati ule kulikuwa na kiungo mshambuliaji anaitwa Omary Hussein , huyu jamaa alikuwa anajua mpira na ndiye alitoa pasi iliyozaa bao kwa Tino,” anasema Idi Pazi.

Kipa huyo anasema mbali na Stars, zilipokutana Simba na Yanga, aliombea sana Omary Hussein asipangwe, kwani alikuwa anamsumbua mno langoni yeye Pazi akiwa kipa wa Simba, kwani alikuwa ni mchezaji mwenye kasi na mbinu nyingi za mpira, kifupi alikuwa anajua.

“Pazi hakuwa naarufu kama Tino kwani tofauti yao, Tino alikuwa mshambuliaji kama ambavyo unamuona Meddie Kagere na Omary Husein alikuwa kama Shiza Kichuya, hivyo anayeonekana sana ni Kagere lakini huyu Omary Hussein alikuwa fundi, Yanga ilipata mchezaji,” anasema.

STARS YA WAKATI ULE ILIKUWA HIVI

Idi Pazi anasema, licha ya kwamba rais wa nchi wakati ule, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hakuwa mpenzi sana wa soka, lakini alitoa fursa kwa mashirika ya Serikali kuwa na timu za mpira.

“Kulikuwa na mashirika kama Pamba, RTC, Reli,Bandari na mengine mengi yalikuwa na timu za mpira, wakati huo ukicheza soka kwenye timu unakuwa ni miongoni mwa wafanyakazi wa timu, hivyo unalipwa mshahara na Shirika.

“Hii ilichangia soka letu kuwa juu, kwani mashirika hayo yalikuwa na timu nzuri sana za soka, wachezaji walitunzwa na mashirika hasa ukute bosi wa Shirika anapenda mpira, basi mchezaji utafurahi,” anasema.

USAJILI WAKE SIMBA NI MSHAHARA WA BAKHRESA

Idi Pazi anakumbuka namna alivyosajiliwa bure kwenye kikosi cha Simba ambacho alicheza kama mfanyakazi wa Bakhresa ambaye ndiye alikuwa akimlipa mshahara wa kipindi chote alichokuwa Simba.

Kipa huyo ambaye alianza soka miaka ya 1970 kabla ya kusajiliwa na Bandari Mtwara mwaka 1977 na kwenda Majimaji ya Songea 1979 anasema alijiunga Simba mwaka 1982.

“Wakati ule nilisajiliwa na Simba kama mtumishi wa Said Bakhresa, hivyo wakati nacheza Simba, sikuwa nalipwa na Simba, mshahara nilikuwa nalipwa na Bakhresa kama mtumishi wake hadi mwaka 1985 nilipoondoka kwenda Suda kucheza soka la kulipwa.

Anasema alirejea nchini kwa lengo la kurudi Simba mwaka 1989, lakini mabosi wa wakati huo pale Msimbazi wakamgomea.

“Niliamua kujiunga na timu ya Prisner baada ya Simba kunikataa, ambako nilicheza hadi 1991 mwishoni ambako Simba walinirejesha baada ya kupata uongozi mpya.

Anasema Prisner ilitaka Simba iwalipe Sh 600,000 kama fedha ya uamisho wake wakidai wamemhudumia vitu vingi, Simba walikubali na yeye kununuliwa na Simba kwa mara ya pili na kuvunja mkataba na Plisner ambayo ililipwa Sh 600,000 kama fedha ya uamisho wake, fedha iliyotolewa na Muarabu mmoja mnazi wa Simba aliyemtaja kwa jina moja la Ahmed na Prisner kumuachia mwaka 1991 akarejea Simba.

Je, anakumbuka kitu gani Simba, ishu ya kushuka daraja ikoje na vipi kuhusu mtu aliyemshawishi Mohamed Mwameja kwenda kukipiga Msimbazi? Hakikisha unafuatilia mwendelezo wa makala haya Alhamisi ijayo kuona mengi kuhusu staa huyu fundi wa soka.