Huyu Grealish ni wa Ligi ya Mabingwa

Birmingham, England. JANA usiku Aston Villa ya Mbwana Samatta ilikuwa uwanjani kusaka alama tatu muhimu mbele ya Manchester United, ili kufufua matumaini ya kuendelea kubaki Ligi Kuu England.

Lakini, Jonathan Barnett ambaye ni wakala wa nahodha wa Aston Villa, Jack Grealish amefichua kuwa mteja wake anaweza kuachana na wababe hao wa Villa Park ili kusaka timu itakayomfanya kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kwa muda mrefu Manchester United imekuwa ikihusishwa na mpango wa kunasa huduma ya Grealish na kauli ya wakala wake ni ishara kwamba, kiungo huyo mshambuliaji yuko njiani hasa wakati huu ambao Villa iko kwenye janga la kushuka daraja.

Hata hivyo, mbali na Man United, mahasimu wao Manchester City hivi karibuni na wenyewe walihusishwa na mpango wa kuisaka saini ya Grealish.

Man City ya Pep Guardiola iko njiapanda kuhusu ushiriki wake kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao ikisubiri uamuzi wa rufani yake na hilo limewafanya baadhi ya mastaa wake kufikiria kuondoka kama watagonga mwamba.

Manchester United imetenga pauni 50milioni kwa ajili ya kumbeba Grealish mwishoni mwa msimu huu ili kwenda kuongeza makali kwenye kikosi chake.

Lakini, Barnett alisema kipaumbele cha kwanza kwa mteja wake kwa sasa ni kuhakikisha Villa inabaki kwenye kipute cha Ligi Kuu England msimu ujao.

“Sidhani kama Villa itashuka daraja msimu huu, wachezaji wanapambana kuhakikisha timu inabaki na Jack anaamini hilo ndio sababu anapambana sana.

“Lakini, kwa upande mwingine nadhani kwa umri wake na ubora alionao kwa sasa itakuwa jambo jema kama msimu ujao atacheza Ligi ya Mabingwa Ulaya ili kukuza zaidi kiwango chake na uzoefu wa michuano mikubwa. Kwa sasa sina uhakika atakuwa sehemu gani msimu ujao, ila hakuna kitakachofanyika kwa sasa kwa kuwa, mkakati ni kuikoa Villa tu isishuke daraja msimu ujao,” alisema.