Huyo Yondani ndo kwanza ananoga

Friday May 17 2019

 

By OLIPA ASSA

SAWA, umri unazidi kumtupa mkono akiwa miongozi mwa wachezaji wakongwe katika Ligi Kuu Bara, lakini unaambiwa beki, Kelvin Yondani kwa jinsi alivyo na ubora wa hali ya juu ndio kwanza ananoga kwani anazeeka na utamu wake.

Hayo yamesemwa na winga wa zamani wa Yanga anayekipiga kwa sasa Ruvu Shooting, Emmanuel Martin ambaye amekiri Yondani ni bonge la beki na kuuma sikio uongozi wa Jangwani kufanya mipango ya kutafuta mbadala wake mapema ili wasije kupata tabu.

Martin alisema Yondani (34) anazeeka na soka lake mguuni, huku akiwa pia na akili za mpira kichwani, kiasi katika safu nzima ya kikosi cha Yanga hakuna anayempata ndio maana akikosekana pengo lake ni rahisi kuonekana.

Alisema beki huyo ana vitu viwili vya kipekee vinavyomtofautisha na mabeki wengine wa Ligi Kuu Bara, kwanza huwa hasitisiti kufanya maamuzi yake na mtulivu eneo la hatari.

“Unajua Yanga wanaweza wakamuona Yondani kama mchezaji wa kawaida, ila kwetu washambuliaji tunajua jinsi anavyotutibulia mipango ya kufunga, Yanga isipomuandaa mapema mbadala yake wakiachana naye watapata tabu sana. Watayumba,” alisema.

Martin alisema hata katika mechi yao iliyopita dhidi ya Yanga na kulala 1-0, kikwazo kwao alikuwa Yondani kwani alikuwa akitibua mambo, sambamba na kuwadhibiti wasiweze kumfikia Klaus Kindoki.

Advertisement

Naye winga Khamis Mcha ‘Vialli’ alisema mabeki wa Yanga wapo imara, lakini kwenye ufundi wanasubiri kwa Yondani aliyedai anawajibika kwa asilimia 100 awapo uwanjani.

“Anajua kuifanya kazi yake kikamilifu, sio beki ambaye mchezaji unaweza ukamvaa kirahisi anapokuwa mbele yako, umri wake unaenda ndio kwanza naona maarifa yake yanaongezeka,” alisema Vialli na kuongeza;

“Tofauti yake na mabeki vijana waliopo ndani ya timu hiyo ni mtulivu, anaamini maamuzi yake ndio maana hachezi kwa presha hata pasi zake zinafika mwisho, ukimuona kuna wakati anapandisha mashambulizi.”

“Anauheshimu mpira ndio maana unamheshimu, kiwango chake kipo vilevile hakishuki hovyo kama wengine, Yanga wasome majira ya kumuandaa mapema mbadala wake,” alisema. Yondani aliyejiunga Yanga mwaka 2012 akitokea Simba, amekuwa mhimili mkuu wa ngome ya timu hiyo.

Advertisement