Huko Jangwani kumenoga

YANGA wanajua kwa msimu wa pili ujao hawatashiriki mechi za kimataifa, lakini hilo halijawafanya kujipunja, kwani ile Kamati ya Uhamasishaji na Uchangishaji fedha imejipanga kinoma.

Wakianza kuhesabu saa tu kabla ya kufanyika ile harambee yao inayoambatana na dhifa maalum pale Serena Hoteli, lakini utamu ni kuwa kila mtu ameichangamkia.

Kamati hiyo ya Yanga ilitoa kadi kwa wanachama huku kila mmoja ikiwa na thamani ya Sh 1 milioni kwa lengo la kuvuna Sh 1.5 bilioni na sasa mchakato umefikia patamu. Ikiwa imeandaa Iftar Gala Dinner na kuweka viwango vya kununua meza ili fedha zitakazopatikana zichanganywe za zile za harambee kuifanya Yanga kufanya usajili wa kishindo na tishio.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Anthony Mavunde alisema michakato yote waliyoianza kuchangia timu yao inakwenda vizuri.

“Kiukweli mambo yote yanakwenda vyema na wanachama wanatoa pesa, licha ya kuwa nipo nje muda katika kusimamia yupo mtu, ambaye anahakikisha kila kitu kinakwenda sawa,” alisema Mavunde, ambaye ni Mbunge wa Dodoma mjini. Kuhusu Iftari Gala Dinner itakayofanyika Mei 18, alisema kila kitu kiko vizuri na wanachama wananua meza.

“Tumepanga idadi ya meza 40 na hadi sasa meza za Sh 1 milioni zinakaribia kwisha, hivyo tumetoa kadi kwa muda mchache, na muitikio ni mkubwa,” alisema Mavunde na kuongeza:

“Kwa wale tuliowagawia kadi za kununua wanaendelea kulipa, hii Iftar kuna mtu anayesimamia na kila anapokwenda kuweka pesa baneki tunajua, hizi fedha zote zinakwenda moja kwa moja kwenye akaunti, hakuna itakayoishia mikononi kwa mtu. Tunaijenga Yanga mpya hatari zaidi.”