Hizi hapa sifa za Mtemi Ramadhan ndani ya Simba

Muktasari:

Fuatilia kesho katika mfululizo wa kuwatambulisha wagombea waliojitokeza wanaotarajia kuanza kampeni wiki ijayo. Klabu ya Simba inatarajia kufanya uchaguzi wake mkuu Novemba 3 baada ya Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) kuziagiza klabu kongwa za Simba na Yanga kufanya uchaguzi wao.

JUZI Jumanne tumeanza mfululizo wa kutambulisha wasifu wa wagombea waliojitosa kwenye Uchaguzi Mkuu wa Simba utakaofanyika Novemba 4 mwaka huu na kulianza na Swedi Mkwabi anayewania nafasi ya Mwenyekiti yenye wagombea wawili.
Katika muendelezo wa makala za kuelekea uchaguzi huo unaosaka Mwenyekiti na Wajumbe wa kamati ya Utendaji watakaoingia kwenye Bodi, leo tunamuaangalia mgombea mwingine wa nafasi ya Mwenyekiti, Mtemi Ramadhani.
Mtemi, nyota wa zamani wa kimataifa wa Simba na Taifa Stars aliyekuwa kwenye kikosi kilichoeshiriki mara ya kwanza na mwisho katika Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 1980 ni kati ya wagombea 19 wanaoshiriki uchaguzi wa Simba.
MTEMI NI NANI?
Mtemi Ramadhani Mangi alizaliwa Novemba 25, 1956 jijini Dodoma, alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Rugambwa kuanzia 1962-68 kisha alijiunga na elimu ya Sekondari 1969-1972 Shule ya Dodoma na baadaye kujiunga na Chuo cha Ushirika Moshi (1965-75).
Alipohitimu chuo hicho cha Ushirika alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (1985-88) alipochukua Shahada ya Kwanza ya Biashara.
Mtemi alifanyakazi katika ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma (1976-79) baadaye alikuwa mtumishi wa Umma (1980-1996) kote huku alikuwa karani.

MZOEFU WA SOKA
Mwaka 1976 hadi 1979 alikuwa mchezaji wa timu iliyoundwa na wachezaji kutoka ofisi ya Waziri Mkuu Dodoma, baadaye alijiunga na Simba mwaka 1980-85 huku pia akiichezea timu ya Taifa, Taifa Stars.
Akiwa nyota wa Simba na Taifa Stars alikuwa kwenye kikosi cha Stars kilichoshiriki michuano ya Afcon 1980 nchini Nigeria na kuanzia mwaka 1997 -2000 alikuwa ni Mwenyekiti wa timu ya Tanzania Stars FC iliyowahi kuiwakilisha Tanzania mara mbili mfululizo katika michuano ya Kombe la Washindi Afrika 1997 na 1998.
Mwaka 2006, Mtemi alikuwa Mtendaji Mkuu wa Moro United na baadaye 2008- 2013 alikuwa Mkurugenzi wa Utawala na Uanachama wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) ambapo mwaka jana aligombea nafasi ya Makamu wa Rais wa TFF ila kura hazikutosha.
Je, unawajua wagombea wa nafasi ya Ujumbe wa Kamati ya Utendaji katika uchaguzi huo wa Simba? Fuatilia kesho katika mfululizo wa kuwatambulisha wagombea waliojitokeza wanaotarajia kuanza kampeni wiki ijayo.