Himid Mao, Zayd wanasikilizia mabosi tu

VIONGOZI wa Shirikisho la Soka Misri, wanatarajiwa kuwa na kikao na Amr Al-Ganaini, ambaye ni mkuu wa kamati inayoendesha Ligi Kuu ya Misri, EFA, na Waziri wa Vijana na Michezo, Dk Ashraf Sobhi, kujadili tarehe ya kurejea kwa ligi za madaraja mbalimbali nchini humo.

Shughuli za kimichezo nchini Misri ambako wapo wachezaji wawili wa Kitanzania, Himid Mao ‘Ninja’ (ENPPI SC) na Yahya Zayd wa Ismaily, ambaye anakipiga kwa mkopo Pharco FC, zilisitishwa Machi mwaka huu, kutokana na kuenea virusi vya corona.

EFA ilitoa taarifa ikisema kwamba, Dk Sobhi atashiriki kikao hicho ambacho kinatarajiwa kutoa mwelekeo wa kurejea kwa ligi huku klabu zikitakiwa kujiandaa kwa mazoezi kuanzia Juni 15, mwaka huu, baada ya siku chache zilizopita kutangaza kuendelea rasmi kwa shughuli za michezo.

Kwa mujibu wa Himid, ambaye anacheza soka la kulipwa nchini humo, alisema kuna baadhi ya mambo ambayo viongozi hao wanaenda kuyajadili kuhusu urejeo wa shughuli hizo za kimichezo.

“Mechi zichezwe katika viwanja ambavyo vipo karibu na sehemu ambazo klabu zimeweka kambi. Kupunguza idadi ya wachezaji kwenye basi moja la timu, kila mchezaji anatakiwa kukaa kiti tofauti, na basi inapaswa kubeba watu 25 badala ya 50.

“Kupunguza idadi ya watu ambao watakuwa wakikaa katika mabechi ya ufundi kwa timu zote wakati wa mechi.

Wachezaji wote wanatakiwa kupimwa na virusi vga corona kabla ya kuendelea na Ligi.

“Ndani ya chumba kimoja cha hoteli anatakiwa kukaa mchezaji mmoja, lakini pia itakuwa marufuku kwa wachezaji na hata makocha au viongozi kushikana mkono na kushangilia pamoja,” alisema.\Chama la Himid, ENPPI FC lipo nafasi ya saba katika msimamo wa Ligi Kuu Misri wenye jumla ya timu 18, wakiwa na pointi 25 walizovuna katika michezo 18.