Hii ya Manchester City wataisoma namba TU

MANCHESTER, ENGLAND. NOMA sana. Manchester City huenda ikawa na siku 14 tu za kujiandaa na msimu mpya kama watafika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Septemba 12 inatajwa kwamba itakuwa mwanzo wa msimu mpya wa 2020-21 kwenye Ligi Kuu England. Lakini, hiyo itakuwa wiki mbili tu mbele baada ya kupigwa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, iliyopangwa Agosti 29.

Na hilo linaweza kukisababishia kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola kutumikia karibu mwaka bila ya kuwa na maandaalizi yanayofaa katika kipindi cha majira ya kiangazi.

Wapinzani wao Liverpool wameshatupwa nje ya Ligi ya Mabingwa Ulaya na Kombe la FA na kubaki kwenye Ligi Kuu England, pekee ambayo msimu wake utamalizika kwenye wikiendi ya Julai 25. Jambo hilo litamfanya Jurgen Klopp na mastaa wake kuwa na wiki saba za mapumziko, wiki tano zaidi ya Man City, ambao bado wapo kwenye mapambano ya kusaka mataji mawili.

Hilo linadaiwa kwamba linaweza kuwa na faida kubwa kwa mabingwa watarajiwa wa Ligi Kuu England kwenye kutetea taji lao hilo msimu ujao.

Ugumu kama huo unaowakabili Man City unaweza kuwahusu pia Manchester United na Wolves, ambao wote bado wanachuana kwenye Europa League. Fainali ya michuano hiyo itapigwa Agosti 25, hivyo nao watakuwa na muda usiozidi wiki mbili katika maandalizi ya msimu mpya kama watafika fainali.

Chelsea itahitaji kufanya maajabu kupindua matokeo ya kuchapwa 3-0 na Bayern Munich kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ili kusonga mbele, huku Man City wao wakipewa nafasi kubwa baada ya kushinda ugenini kwa Real Madrid na msimu huu wanaonekana kuwa na nguvu kubwa kwenye kuubeba ubingwa.

Winga wa miamba hiyo ya Etihad, Riyad Mahrez anaamini huu ni mwaka wao wa kutamba Ulaya na kusema: “Tuna timu, tuna kocha, tuna kila kitu na tupo vizuri kiasi cha kutosha kushinda ubingwa.”