Hii ndio siri ya Mdamu kwenda Kenya

Monday February 18 2019

 

BAADA ya kujiunga na Kariobangi Sharks kwa kandarasi ya miaka mitatu akitokea Singida United, Athanasi Mdamu amesema yuko tayari kuanza maisha yake mapya ya soka Kenya.

Mdamu alisema nafasi aliyopata ya kucheza soka Kenya inaweza kumfanya siku moja kuitwa Taifa Stars kama ilivyokuwa kwa kiungo wa Bandari, Abdallah Hamis.

“Ligi ya Kenya ni nzuri pia ina ushindani ndio maana klabu zao zimekuwa zikitusumbua na hata timu yao ya taifa, ushindani wao naamini utaimarisha kiwango changu,” alisema nyota huyo.

Mdamu amekwenda Kenya baada ya Kariobangi Sharks kumuona na kumpenda kupitia michuano ya Sportpesa iliyofanyika mwaka huu Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Singida United, Festo Sanga alisema viongozi wa Sharks waliwasiliana na klabu yao na kukaa chini na kutoa uamuzi wa kumruhusu mchezaji huyo.

“Lengo letu ni yeye aende kuongeza maarifa kwa faida yake na taifa kwa jumla, tutaendelea kushirikiana naye huko aendapo, tumeishi naye vizuri na ni kijana anayejitambua,” alisema Sanga

Sanga aliongeza huo ni mwendelezo wa programu zao za kuwaruhusu wachezaji kwenda kucheza soka nje ya nchi pale tu wanapopata timu kama ambavyo mkataba wa timu na mchezaji unavyoeleza.

“Tunategemea mchezaji mwingine kuondoka siku za karibuni kwenda kucheza barani Ulaya na taratibu zake zote zimeshakamilika.”

Advertisement