Hazard: Hata nafasi ya tano poa tu aisee

Friday April 13 2018

 

LONDONENGLAND


SUPASTAA Eden Hazard amesema itakuwa kitu kizuri sana kama Chelsea itashindwa kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Wakati wengi wakidhani itakuwa aibu kubwa kwa wababe hao wa Stamford Bridge wakishindwa kufuzu kucheza michuano ya Ulaya, lakini Hazard amekuwa na mtazamo tofauti akisema ni bora iwe hivyo.

Chelsea imeshatupwa nje ya michuano ya Ulaya kwa msimu huu na haionekani kuwa na nafasi ya kukamatia nafasi hiyo kwa msimu ujao baada ya sasa kushika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, pointi 10 nyuma ya timu inayoshika nafasi ya nne, Tottenham Horspur.

Hilo likitokea, ina maana kwa msimu ujao Chelsea itakuwa kwenye Europa League na Hazard anaamini hilo litakuwa jambo bora kwa sababu watatuliza akili yao kwenye ligi na kufanya vizuri kama ilivyotokea kwenye msimu wake wa kwanza wa Antonio Conte kwamba Chelsea haikuwa na michuano mingi na matokeo yake ilibeba Kombe la ligi kiulaini tu.

“Naamini kwa mashabiki wetu na sisi wenyewe, tutafikia mafanikio fulani,” alisema Hazard.

“Bado tupo kwenye Kombe la FA na tunahitaji kuleta taji Stamford Bridge mwishoni mwa msimu. Unapokuwa Chelsea itahitaji ucheze Ligi ya Mabingwa Ulaya kila mwaka, lakini mwaka jana hakutucheza na tulishinda ubingwa wa ligi, hivyo wakati mwingine kitu kibaya kinaleta kitu kizuri. Hata hivyo, hatujakata tamaa tunacheza kwa ajili ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kuna mechi sita zimebaki kwenye ligi na tutajaribu kufanya kila tunaloweza hadi kufika mwisho wa msimu.”