Hata kwa ungo... Kagere, Chama Lazima ndani

SIMBA imesisitiza kwamba itapambana kwa namna yoyote ile kuhakikisha mastaa wake walioko nje wanatua kabla ya Ligi Kuu Bara kuendelea baadaye mwezi ujao.

Habari za uhakika zinadai kwamba Ligi hiyo huenda ikaanza wiki ya pili ya Juni kwa viporo vya Yanga na Simba.

Wachezaji wa Simba walioko nje ya mipaka ya Tanzania ni Clatous Chama (Zambia), Francis Kahata (Kenya), Sharaf Shiboub (Sudan) na Meddie Kagere (Rwanda).

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Senzo Mazingisa ameiambia Mwanaspoti jana kwamba wameziandikia barua mamlaka za nchini husika wakiomba ruksa kwa wachezaji hao wapenye angalau kwa magari mipakani.

“Tumeandika barua kwa mamlaka za nchi hizo walipo wachezaji wetu kuomba angalau waachiwe wafike mipakani waangalie uwezekano wa kuingia nchini,” alisema Senzo.

“Wakisharuhusiwa kutoka nje ya mipaka tutajua jinsi ya kuunganisha iwe kwa basi, usafiri binafsi au ndege,” alisema kiongozi huyo.

Alisema kwamba kama wakifanikiwa kurudi nchini kwa wakati watawafanyia vipimo na kuchukua tahadhari zote za kiafya.

“Tuna uhakika kama mambo yakienda vizuri tunaweza kuwa nao kabla ya ligi haijaanza,” aliongeza ingawa huenda ikawa ngumu zaidi kumpata Shiboub kwavile kwao amri ya kutotoka nje imetiliwa mkazo sana na mamlaka zote.

Kiongozi huyo aliwatoa wasiwasi mashabiki na kusema kwamba Simba iko imara na itaimarika zaidi kwani wachezaji hao kuna uwezekano wakawepo.

Aliongeza kwamba hata kama watakosekana kwenye mechi za awali ana uhakika Simba haitayumba kwani imesajili kikosi kipana chenye machaguo mengi.

Serikali imeruhusu ligi ziendelee kuanzia Juni mosi ambapo mamlaka za soka zimeshajipanga kwa utaratibu wa kuchezwa kwenye vituo viwili.

Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho zitachezwa Dar es Salaam kwenye viwanja vya Uhuru, Taifa na Chamazi huku Daraja la Kwanza na La pili zikichezwa Mwanza ndani ya Nyamagana na Kirumba.

Lakini habari za ndani kutoka kwenye kikao cha Wizara na wadau juzi na jana, zinadai kwamba baadhi ya wadau wanataka mfumo wa nyumbani na ugenini uendelee licha ya kwamba wenye mamlaka ya mwisho ni serikali na huenda tamko jingine likatoka kesho kuhitimisha mjadala huo mrefu wa uendeshaji ligi.