Hasunga: Miss Journalism World kumekucha

Thursday September 13 2018

 

By Mwandishi Wetu

Dodoma. Taasisi pamoja na watu binafasi wametakiwa kuliunga mkono shindano la Miss Journalism World 2018, litakalofanyika Desemba mwaka huu jijini Arusha na kushirikisha washiriki kutoka nchi zaidi ya 60, kwa kujitokeza kulidhamini kwani litaitangaza Tanzania katika ngazi ya kimataifa haswa katika sekta ya utalii.

Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga, wakati wa kuzindua tiketi za kidiplomasia katika hafla iliyofanyika New Dodoma Hotel juzi usiku mjini hapa.

Hasunga alisema, katika kipindi hiki ambacho Tanzania inapigana katika kujitangaza katika sekta ya utalii, inafurahisha zaidi kuona kuna ubunifu mkubwa kutoka kwa wadau mbalimbali katika kuhakikisha nchi yetu inajulikana zaidi kimataifa.

“Nyumbani kumenoga, napenda kuwaomba wadau mbalimbali kujitokeza kuliunga mkono shindano hili, kwani kwa kushirikisha washiriki kutoka nchi zaidi ya 60 ni faida kubwa kwetu, haswa katika sekta ya utalii.

“Katika kipindi hiki ambacho kuna ushindani mkubwa katika sekta ya utalii, napenda kuwafahamisha Tanzania ni moja kati ya nchi chache duniani zenye vivutio vya kutosha na tunapigana ili kuendelea kutangaza vivutio vingi tulivyonavyo,” alisema.

Naye Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Anthony Mavunde, ambaye pia ni Mbunge wa Dodoma Mjini (CCM), alikiri kufurahishwa kwake na uwepo wa shindano hilo na kusema ni fursa kwa Tanzania kuendelea kujitangaza zaidi.

“Nimefurahi uzinduzi huu kufanyika hapa Dodoma na ninawakaribisha sana, ila hii ni fursa kubwa kwetu kama Taifa kuendelea kujitangaza kimataifa zaidi kupitia sekta ya utalii,” alisema.

Mratibu wa shindano hilo, Samwel Chazi alisema, kwa sasa shindano hilo ni moja kati ya mashindano makubwa duniani, kutoka na kushirikisha washiriki wengi zaidi kutoka mataifa mbalimbali.

“Bado kuna changamoto kadhaa na pia tunashukuru kwa sapoti kubwa tunayoipata kutoka serikalini, lakini tunaendelea kuomba wadhamini zaidi wajitokeze kwa ajili ya kulidhamini shindano hili,” alisema.

Uzinduzi huo ulihudhuriwa pia na Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Godfrey Mngereza, viongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, mwakilisi wa Kamanda wa Polisi Mkoa, wabunge na watu wengine maarufu ulisindikizwa na burudani ya muziki kutoka bendi ya Mjengoni Classic ya Arusha.

Shindano la Miss Journalism World litafanyika katika hoteli ya Ngurdoto, Arusha Desemba mwaka huu, huku kukiwa na vipengele kadhaa vya kushindaniwa.

Advertisement