Hapana chezea Simba wewee!

MASHABIKI wengi wa Simba bado wanaweweseka kwa furaha baada ya chama lao kuandikisha rekodi mpya katika Ligi Kuu Bara msimu huu walipoifumua Coastal Union ya Tanga kwa mabao 8-1.

Hata hivyo watani zao, Yanga wanaibeza Simba kwa ushindi huo dhidi ya Wagosi kwa kuamini kuwa waliifunga timu dhaifu iliyokuwa imeelemewa na uchovu wa safari kwani walitua saa chache kabla ya kuvaana na Mnyama kwenye Uwanja wa Uhuru, jijini Dar.

Katika mchezo huo, washambuliaji nyota wa Simba, Mganda Emmanuel Okwi na Meddie Kagere kutoka Rwanda kila mmoja akiibuka shujaa kwa kufunga hat trick jambo ambalo liliamsha shangwe kwa mashabiki wa timu hiyo kuona mashujaa wao wapo moto kinoma.

Kila mtu amezungumza yake juu ya kipigo hicho, lakini kumbe usichokijua tu ni kwamba Simba huwa inajua kugawa vipigo vya maana tu ikimpata mpinzani aliyejichanganywa kwao.

Makala haya yanaangazia vipigo sita vya maana ambavyo Simba imetoa kwa wapinzani wao katika miaka ya karibuni.

SIMBA 6-0 MGAMBO SHOOTING

Huu ulikuwa msimu wa 2013-2014 ambapo ulianza kwa kishindo kwa Simba kwani baada ya mechi tatu tu ilikuwa tayari imeshikilia usukani wa Ligi. Hata hivyo mchezo wa kusisimua zaidi ulikuwa dhidi ya Mgambo Shooting ya Tanga, uliopigwa Sept 18, 2013. Katika mchezo huo Simba ilivuna karamu ya mabao baada ya kuitungua Mgambo 6-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Nyota wa mchezo huo alikuwa straika Mrundi, Amissi Tambwe aliyefunga mabao manne na kupeleka shangwe Msimbazi.

SIMBA 6-1 MAJIMAJI

Kipigo kingine cha maana kutoka kwa Simba katika siku za karibuni kiliwaangukia Majimaji Songea iliyonyooshwa mabao 6-1 katika pambano la upande mmoja lililopigwa Oktoba 31, 2015. Ushindi huo uliibua shangwe na nderemo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya Wekundu wa Msimbazi hao kuvuna karamu hiyo ya mabao. Nyota wa mchezo huo alikuwa mshambuliaji raia wa Uganda, Hamis Kiiza aliyefunga mabao matatu ‘hat trick’ na kuwafanya Majimaji kulala mapema.

SIMBA 5-0 PRISONS

Hawa Simba achana nao kabisa kwani ishu za kugawa dozi haijalishi wanagawa kwa timu ipi, kwani hata maafande wa Magereza, Tanzania Prisons nao walishaonja shubiri.

Prisons ya Mbeya ilikumbana na dhahama ya kupigwa ‘mkono’ kwenye mchezo wao wa Februari 28, 2015 kwa kufungwa mabao 5-0.

Mchezo huo ulichezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam siku moja tu kabla ya kufanyika kwa Mkutano Mkuu wa Simba na kipigo hicho kilikuwa kama zawadi kwa wanachama na mashabiki hao kabla ya kukutana kwenye mkutano huo. Nyota wa mchezo huo alikuwa Ibrahim Ajibu aliyefunga mabao matatu ‘hat trick’.

SIMBA 5-0 YANGA

Yanga wanakejeli ushindi wa watani zao kuwa wameiotea Coastal ikiwa chovu, lakini huenda wamesahau kuwa, hata wao nao walishakumbana na makali ya mnyama.

Ndio, kipigo kingine cha maana kutoka kwa Simba kilikwenda kwa Yanga na pengine Jangwani hawataki kukikumbuka kwani nao walinyooshwa 5-0 kwenye Uwanja wa Taifa.

Kipigo hicho kilijiri siku ya Simba kukabishiwa taji lao ubingwa waliotwaa mapema msimu wa 2011-2012 na mechi ikuipigwa Mei 6, 2012 ambapo Emmanuel Okwi alifumania nyavu mara mbili, huku marehemu Patrick Mafisango, Juma Kaseja na Feluix Sunzu kila mmoja akitupia kambani bao moja.

SIMBA 5-0 RUVU SHOOTING

Simba buana haina utani ikitaka kumtia mtu aibu, kwani Ruvu Shooting msimu huu wamekumbana na kipigo cha aibu toka kwa Wekundu hao.

Simba ikitoka kuinyoosha Alliance ya Mwanza kwa mabao 5-1, ambapo Okwi alitupia mabao mawili, Ruvu nao waliingia kichwakichwa na kupigwa mkono na Msimbazi.

Katika mchezo huo uliopigwa Oktoba 28, mwaka jana tu, Okwi akicheka na nyavu mara tatu yaani akitupia hat trick yake ya kwanza msimu huu.

SIMBA 7-0 RUVU SHOOTING

Hili lilikuwa pambano la kwanza la msimu uliopita ambapo Ruvu wakiwa na kikosi cha vijana, baada ya nyota wake wengi kwenda mafunzo ya kijeshi Zanzibar walikutana na dhahama. Walipigwa ‘wiki’ na Mnyama kwenye Uwanja wa Taifa, katika pambano hilo lililopigwa Agosti 27, 2017 ambapo Okwi aliwavuruga kabisa maafande hao kwa kutupia kambani mabao manne pekee yake na kuifanya Ruvu kuanza msimu na mkosi.

Kabla ya pambano hilo, Msemaji wa Ruvu, Masau Bwire alichonga sana, lakini baada ya kipondo hicho alipotea kimya kimya na kufanya mashabiki wa Simba kudai eti ukiona Simu za Masau ujue Simba kamla....Simba waliinyoosha vibaya sana Ruvu.