Hans Poppe akiri kuhusika ununuzi nyasi za Simba

Muktasari:

Hans Poppe alifikishwa mahakani hapo kwa mara ya kwanza wiki iliyopita baada ya kurejea nchini na kukamatwa na Takukuru akiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Mfanyabiashara na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu ya Simba, Zacharia Hans Poppe, amekiri mahakamani kuhusika na mchakato wa ununuzi wa nyasi bandia kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa klabu hiyo, ulioko Bunju, Kinondoni Dar es Salaam.

Hans Poppe amekiri uhusika huo, wakati wa kusomewa maelezo ya awali (PH) wa kesi inayomkabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, yeye na vigogo wengine wawili wa klabu hiyo, Rais Evans Aveva na makamu wake, Geofrey Nyange 'Kaburu', baada ya kusonewa maelezo ya kesi hiyo.

Kesi hiyo inatokana na matumizi ya fedha za uhamisho wa mshambuliaji wa klabu hiyo, Emmanuel Okwi, kwenda Etoile Sportive Du Dahel, ya Tunisia, kwa madai ya kutumia pesa hizo kununulia nyasi bandia na gharama za ujenzi wa uwanja huo.

Katika kesi hiyo Hans Poppe anakabiliwa na mashtaka mawili, ya kughushi nyaraka na kuwasilisha nyaraka za uwongo yeye pamoja na wenzake.

Aveva na Kaburu wanakabiliwa na mashtaka mengine zaidi ya matumizi mabaya ya madaraka kwa kuhamisha fedha hizo bila mamlaka ya Kamati ya Utendaji ya Simba, kujipatia pesa isivyo halali (Aveva) na utakayishaji fedha yanayowakabili wote, Aveva na Kaburu.

Washtakiwa Aveva na Nyange wanatetewa na mawakili Nehemia Nkoko na Nestory Wandiba wakati Hanspoppe yeye anatetewa wa Wakili Agostino Shio.

Leo washtakiwa hao walisomewa maelezo ya kesi hiyo na kisha wakatakiwa kuonesha mambo wanayokubaliana nayo na yale wasiyokubaliana nayo.

Hans Poppe alikubali kuhusika katika mchakato wa ununuzi wa nyasi hizo bandia.

Aveva na Kaburu walikubali majina yao na nafasi zao za uongozi ndani ya klabu ya Simba, lakini wakakana maelezo mengine yote.

Upande wa mashtaka kupitia kwa Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro ulisema utaleta na shahidi wengi pamoja na vielelezo lakini bila kutaja idadi ya mashahidi hao.

Akiwasomea maelezo ya awali (PH) Wakili wa Serikali Mwandamizi Shadrack Kimaro akisaidiana na Mutalemwa Kishenyi, alidai kuwa Machi 12, 2016, Klabu ya Simba ililipwa jumla ya Dola za kimarekani 319, 212 na Klabu ya Etoile Sportive Du Sahel ya nchini Tunisia.

Kimaro alidai kiasi hicho cha fedha kilikuwa ni ada ya uhamisho wa mchezaji Emmanuel Okwi kwenda Klabu ya Etoile Sportive Du Sahel ya nchini Tunisia.

"Fedha hizo ziliingizwa katika akaunti ya Klabu ya Simba kupitia akaunti namba O1J1026761800 iliyopo katika Benki ya CRDB tawi la Azikiwe.

Aliendelea kudai mahakamani hapo kuwa, Aveva na Nyange ndio waliokuwa watiaji saini wa akaunti hiyo.

Kimaro aliendelea kudai kuwa baada ya malipo hayo,  Machi 15, 2016 kiasi hicho cha Dola 300,000 kilihamishwa kwenda akaunti namba 147002211 ya benki ya Barclays iliyopo tawi la Ohio.

aliongeza kuwa akaunti hiyo iliyokuwa katika Benki ya  Baclays ni akaunti binafsi ya Aveva, ambayo yeye pekee ndio mtiaji saini.

"Uhamisho wa fedha hizo kwenda katika akaunti binafsi ya Aveva, ulitumia fomu ya kuhamisha fedha ya Machi 15, 2016,  ambayo iliwasilishwa benki ya CRDB na Aveva.

Alidai kuwa fomu hiyo ya kuhamisha fedha ilisainiwa na mshtakiwa wa kwanza na wa pili ambao ni Aveva na Nyange na maelezo ya malipo katika fomu hiyo, yalikuwa yanasomeka kama malipo ya mkopo.

Kimaro aliendelea kudai kuwa uhamisho wa fedha hizo haukuwa umeidhinishwa na Kamati ya Utendaji ya Klabu ya Simba na Klabu ya Simba ilikuwa haijawahi kukopa kiasi hicho cha fedha kutoka kwa mshtakiwa wa kwanza (Aveva).

"Baada ya kuingiza fedha hizo katika akaunti binafsi ya Aveva, fedha hizi zilitolewa taslimu kwa mafungu tofauti tofauti na mtia saini ambaye ni Aveva " alidai.

Alibainisha kuwa kati ya Dola za kimarekani 300,000 zilizoingizwa katika akaunti ya Aveva, mshtakiwa huyo alihamisha Dola za kimarekani 62,183 kwenda kampuni ya Ninah Ghuanzhour Trading Co Ltd.

Akibainisha kuwa pesa hizo zilikuwa kama gharama ya kununua nyasi bandia kwa ajili ya uwanja wa michezo wa Klabu ya Simba, uliopo Bunju wilaya ya Kinondoni.

Aliendelea kudai kuwa kiasi kingine cha fedha ambazo ni Dola za kimarekani 50,000, zililipwa kwa Franklin Lauwo kama gharama za ujenzi wa uwanja wa Klabu Simba.

Lauwo ni mmiliki wa Kampuni ya Ranky Infrastructure & Engineering Ltd.

Kimaro alidai mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo, Hanspoppe yeye alikodi Kampuni ya Ranky Infrastructure & Engineering Ltd kufanya Ujenzi wa uwanja huo wakati akijua kuwa kampuni hiyo ilikuwa haujasajiliwa na Bodi ya Wahandisi na Wakandarasi (CRB).

Pia Hanspoppe anawajibika katika kufanya mchakato wa ununuzi wa nyasi bandia.

Kimaro alidai kuwa bila kujali matumizi kwa baadhi ya pesa hizo kwa ununuzi wa nyasi bandia na uhusika wa kampuni ya Rank hiyo, Aveva na Kaburu hawakuweza kutoa maelezo ya Dola za Marekani 187,817 ambazo ziliingizwa kwenye akaunti ya Aveva.

Kimaro alidai kuwa kwa ajili ya kuondoa nyasi bandia zilizokuwa zimeingizwa katika Bandari ya Dar es Salaam, Aveva, Nyange na Hanspoppe walitengeneza hati ya malipo ya uongo namba 201605280001 na kuiwasilisha Mamlaka ya Mapato nchini (TRA).

Alibainisha kuwa hati hiyo ilikuwa inaonyesha thamani ya Nyasi bandia ilikuwa Dola za kimarekani 40,577 na kwamba hati hiyo ilitengenezwa kwa lengo la kukwepa kodi.

Hakimu Simba baada ya kusikiliza maelezo hayo, aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 31, ambapo upande wa mashtaka unaanza kutoa ushahidi.