Hali si shwari Manchester City

Tuesday June 30 2020
city pic

Manchester, England. Inaelezwa kwamba mambo si shwari ndani ya klabu ya Manchester City. Kuna tishio kubwa la baadhi ya wachezaji wa kikosi hicho kutaka kuondoka.

Winga Leroy Sane (pichani) anaweza kukamilisha dili lake la kwenda kukipiga Bayern Munich ya Ujerumani huku kiungo Kevin De Bryune naye akisubiri kuona rufani ya klabu hiyo dhidi ya marufuku ya kutoshiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya itatoka na uamuzi gani, Pep Guardiola naye hajaweka wazi hatima yake ndani ya klabu hiyo.

Kocha huyo aliyeiwezesha kubeba mataji kadhaa yakiwamo ya Ligi Kuu England, Carabao na FA, mkataba wake umebaki mwaka mmoja tu na hakuna mazungumzo mapya mpaka sasa.

Habari za ndani ya klabu hiyo zinadai kuwa Guardiola hana mpango wa kuendelea kuwapo Etihad baada ya msimu ujao huku kukiwa na sintofahamu kuhusu ushiriki wake kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

“Nafurahia kuwa sehemu ya mafanikio ndani ya klabu, tumepoteza msimu huu, lakini tunajipanga vyema kuwakabili Liverpool msimu ujao,” alisema alipoulizwa kuhusu mikakati yake ya baadaye.

“Nitafanya kwa uwezo wangu ili kuwa na mafanikio. Lakini, sitaki kufikiria mipango ya mbali zaidi. Kwa sasa nawaza tuna mechi ngumu mbele yetu.”

Advertisement

Man City inajiandaa kuingia kwa kishindo kwenye soko kutokana na kauli ya De Bruyne huku Sergio Aguero (32), akiwa majeruhi na Raheem Sterling akiwa bado hajasaini mkataba mpya huku Barcelona na Real Madrid wakimsaka.

Advertisement