Haji Mwinyi hana chake Yanga

BEKI wa Yanga, Haji Mwinyi ‘Ngwali’

Muktasari:

  • BEKI Haji Mwinyi Mngwali hana namba ndani ya Yanga na hajacheza hata mchezo mmoja katika Ligi Kuu Bara, jambo lililomfanya ajishtukie kwamba hana chake Jangwani na kujipanga mapema kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili.

BEKI wa Yanga, Haji Mwinyi ‘Ngwali’ aliyeng’ara kikosi hicho kabla ya kupoteza nafasi ya kudumu amekiri mambo yake magumu Jangwani lakini anachoshukuru ni jinsi anavyokiamini kiwango chake.

Mwinyi hajapata nafasi ya kucheza tangu msimu wa Ligi Kuu Bara uanze zaidi ya kucheza katika mechi za kirafiki tu tangu Kocha Mwinyi Zahera aanze kukinoa kikosi hicho.

“Nafikiri ni nyakati tu, sijajua ni kitu gani mwalimu anakitaka lakini utafika wakati wangu nitafanya vizuri. Kitu kikubwa ninachoshukuru ni kwamba sina wasiwasi na kiwango changu,” alisema Mwinyi huku akisisitiza hajakata tamaa.

Amefafanua, kitu kikubwa anachofanya ni kujiweka tayari wakati wote kwa kufanya mazoezi kwa nguvu ili wakati wowote atakapopata nafasi ya kucheza afanye vizuri.

“Binafsi najitambua na najua cha kufanya. Unajua kama ilivyokuwa kipindi kile hapa klabuni sikuwa na nafasi ya kucheza lakini nilipokwenda kwenye Kombe la Chalenji Kenya na Zanzibar Heroes nilifanya vizuri kwa sababu nilikuwa tayari,”alisema Mwinyi na kufafanua ubora wake uliwatamanisha hadi timu nyingine kama Gor Mahia kumuhitaji.

Akifafanua mpango wa kutakiwa na Gor Mahia umefika wapi Mwinyi alisema: “Kipindi kile klabu yangu ilikataa sijui tena kinachoendelea kila kitu kipo mikononi mwa Yanga.”

Hata hivyo, awali Zahera alisema, katika kikosi chake anawapa nafasi wachezaji wanaofanya vizuri mazoezi na si majina; “Siangalii majina ninachoangalia ni uwezo wa kila mchezaji wale wanaofanya vizuri kwangu hawakosi nafasi ya kucheza, iko hivyo.”