HAWA NDO WAMEPIGA PESA NDEFU MWAKA HUU

LONDON, ENGLAND. SUPASTAA wa Barcelona, Lionel Messi ndiye mwanasoka aliyelipwa pesa nyingi zaidi duniani. Mshindi huyo mara sita wa Ballon d’Or hivi karibuni aliingia kwenye vichwa vya habari kwa jambo moja tu - kuripotiwa kutaka kuachana na miamba hiyo ya Nou Camp kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Kwa mujibu wa Forbes hii hapa orodha ya wanasoka waliovuna pesa ndefu zaidi kwa mwaka huu kutokana na malipo ya mishahara pamoja na dili za mikataba ya kibiashara.

10. David de Gea (Man United)

Amelipwa: Dola 27 milioni

Mshahara: Dola 24 milioni

Dili za kibiashara: Dola 3 milioni

Huyu ni kipa pekee kwenye kikosi hiki. Huduma ya David De Gea anayotoa huko Manchester United imemfanya kuwa mmoja wachezaji wanaolipwa pesa nyingi jambo lililomfanya aweke kibindoni mkwanja wa Dola 27 milioni kwa mwaka huu, huku mishahara ikimwingizia Dola 24 milioni na dili za mikataba ya kibiashara zimemwingizia Dola 3 milioni. De Gea ni mmoja wa wachezaji moto kabisa wanaokipiga kwenye Ligi Kuu England.

9. Robert Lewandowski (Bayern Munich)

Amelipwa: Dola 28 milioni

Mishahara: Dola 24 milioni

Dili za kibiashara: Dola 4 milioni

Kiwango cha straika Lewandowski kwa msimu uliomalizika kilikuwa matata kabisa na jambo hilo liliendana na kipato chake cha mwaka, ambapo fowadi huyo wa kimataifa wa Poland aliingiza Dola 28 milioni. Kwenye mkwanja huo, Lewandowski mishahara ilimwingizia Dola 24 milioni, huku dili za mikataba ya kibiashara zilimwingiza Dola 4 milioni na hivyo kuwa miongoni mwa wanasoka waliovuna mkwanja mrefu kwa mwaka 2020 kwa mujibu wa Forbes.

8. Gareth Bale (Real Madrid)

Amelipwa: Dola 29 milioni

Mshahara: Dola 23 milioni

Dili za kibiashara: Dola 6 milioni

Lisemwalo kwa sasa linamhusisha staa Bale na mpango wa kurejea kwenye klabu yake ya zamani ya Tottenham Hotspur kabla ya dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi kufungwa. Real Madrid inataka kuachana na mchezaji huyo ili kupunguza bili ya mishahara, ambapo Bale anaripotiwa kwa mwaka huu amelipwa mishahara ya Dola 23 milioni, huku akiingiza jumla ya Dola 29 milioni. Dili za kibiashara zimemwingizia Dola 6 milioni.

7. Antoine Griezmann (Barcelona)

Amelipwa: Dola 33 milioni

Mshahara: Dola 28 milioni

Dili za kibiashara: Dola 5 milioni

Maisha ya Griezmann huko Barcelona inaweza kuwa tofauti baada ya ujio wa kocha Ronald Koeman, ambaye iliripotiwa kuwa mipango yake ni kutengeneza kikosi kumzunguka fowadi huyo Mfaransa. Ndani ya uwanja Griezmann yupo vizuri kama ilivyo mfukoni, ambapo kwa mwaka huu kwa mujibu wa Forbes amevuna Dola 33 milioni, hukumishahara imemwingizia Dola 28 milioni na dili nyingine za mikataba ya kibiashara zimemwingizia Dola 5 milioni.

6. Paul Pogba (Man United)

Amelipwa: Dola 34 milioni

Mshahara: Dola 28 milioni

Dili za kibiashara: Dola 6 milioni

Mchezaji ghali kabisa kwenye kikosi cha Manchester United ni kiungo Mfaransa, Paul Pogba. Staa huyo mshindi wa Kombe la Dunia ni moja ya wachezaji waliovuna mkwanja mrefu kwa mwaka huu, akiwa amevuna Dola 34 milioni - Dola 28 akivuna kupitia mishahara na Dola 6 milioni aliweka kibindoni kupitia dili zake mbalimbali za mikataba ya kibiashara. Jambo hilo linamfanya Pogba kuwa mmoja wa mastaa wenye pesa ndefu duniani.

5. Mohamed Salah (Liverpool)

Amelipwa: Dola 37 milioni

Mshahara: Dola 24 milioni

Dili za kibiashara: Dola 13 milioni

Liverpool wanatamba kwenye Ligi Kuu England na hilo limekuwa likichangiwa kwa kiasi kikubwa na huduma ya Mohamed Salah. Staa huyo alibeba Kiatu cha Dhahabu cha Ligi Kuu England kwa misimu miwili mfululizo jambo ambalo limemsogeza kwenye dili za pesa ndefu, ambapo kwa mwaka huu amelipwa Dola 37 milioni - mshahara Dola 24 milioni na dili za mikataba ya kibiashara zimemwingizia mkali huyo ya Anfield, Dola 13 milioni.

4. Kylian Mbappe (PSG)

Amelipwa: Dola 42 milioni

Mshahara: Dola 28 milioni

Dili za kibiashara: Dola 14 milioni

Kinachoripotiwa kuhusu Mbappe ni kwamba amewaambia mabosi wa klabu yake ya Paris Saint-Germain kwamba mwishoni mwa msimu huu amepanga kuachana na timu hiyo. Mwenyewe aliripotiwa kutaka kujiunga na Real Madrid. Kama ilivyo mambo yake matamu ndani ya uwanja, hata kwenye mambo ya pochi nene Mbappe yupo vizuri. Kwa mwaka huu amelipwa Dola 42 milioni, mishahara Dola 28 milioni na dili za kibiashara ni Dola 14 milioni.

3. Neymar (PSG)

Amelipwa: Dola 96 milioni

Mshahara: Dola 78 milioni

Dili za kibiashara: Dola 18 milioni

Kwenye orodha ya wanasoka matata kabisa ndani ya uwanja, Neymar amekuwa mmoja wa wakali hao kutokana na mafanikio yake ya uwanjani. Sambamba na ubora wake wa uwanjani, hata kwenye mambo ya pesa pia Neymar amekuwa vizuri, ambapo kwa mwaka huu amelipwa Dola 96 milioni, ambapo mishahara ni Dola 78 milioni na Dola 18 milioni aliingiza kwa kupitia kwenye dili zake za mikataba ya kibiashara.

2. Cristiano Ronaldo (Juventus)

Amelipwa: Dola 117 milioni

Mshahara: Dola 70 milioni

Dili za kibiashara: Dola 47 milioni

Staa, Cristiano Ronaldo hivi karibuni alimvisha pete ya uchumba yenye thamani kubwa sana mrembo Georgina Rodriguez. Na Ronaldo amefanya hivyo kwa sababu tu pesa anayo, ambapo kwa mwaka huu peke yake amelipwa Dola 117 milioni, ambapo mishahara ni Dola 70 milioni na dili nyingine za kibiashara alilipwa Dola 47 milioni na hivyo kushika namba mbili kwenye orodha ya wanasoka waliolipwa pesa ndefu kwa mwaka huu kwa mujibu wa Forbes.

1. Lionel Messi (Barcelona)

Amelipwa: Dola 126 milioni

Mshahara: Dola 92 milioni

Dili za biashara: Dola 34 milioni

Supastaa wa Kiargentina, Lionel Messi ndiye mwanasoka aliyelipwa pesa nyingi zaidi kwa mwaka huu wa 2020. Mkali huyo wa Barcelona, ambaye hivi karibuni aliwatikisa mabosi wa timu hiyo akiwaambia anataka kuondoka kabla ya kubadili mawazo na kubaki kwa mwaka huu amelipwa Dola 126 milioni, ambapo mshahara ni Dola 92 milioni na dili nyingine za mikataba ya kibiashara imemwingizia Dola 34 milioni.