Gwambina yafukuzia rekodi ya Namungo

Dar es Salaam. Kinara wa kundi B katika Ligi Daraja la Kwanza (FDL), Gwambina FC inasaka pointi tisa katika michezo minne iliyobakiza ili kuifikia rekodi iliyowekwa na Namungo FC msimu uliopita.

Namungo FC ilifanikiwa kupanda Ligi Kuu kwa kuongoza kundi A la ligi hiyo ikikusanya alama 49 na kuifanya kuwa mojawapo wa timu zilizopanda kwa kishindo ikiwa na alama nyingi.

Sio tu kwamba ilipanda kwa kishindo, bali hata wapinzani wake, Mlale FC iliwaacha mbali kwa alama 10 baada ya kumaliza msimu kwa kukusanya alama 39 katika michezo 22.

Pia, Namumgo ilifanikiwa kutoa mfungaji bora katika ligi hiyo, Reliants Lusajo, aliyemaliza msimu na mabao 15, ilhali msimu huu nahodha wa Gwambina FC, Jacob Massawe akiwa kinara ana mabao 10 hadi sasa.

Gwambina FC yenye pointi 40 katika michezo 18 huku ikiwa imesaliwa na michezo minne kumaliza msimu, endapo itashinda michezo yote itaifanya kumaliza Ligi Daraja la Kwanza ikiwa na pointi 52.

Katika msimu wa 2018/19, JKT Tanzania ndio timu iliyopanda Ligi Kuu ikiwa na pointi nyingi ambazo ni 37, KMC ikamaliza na pointi 28 na Coastal Union pointi 26.

Gwambina FC wanasaka alama tatu pekee kujihakikishia kucheza Ligi Kuu msimu ujao ikiwa ni moja ya timu ambazo zinamiliki viwanja vyao kwenye ligi hiyo kama ilivyo kwa Ihefu FC inayomiliki Uwanja wa Highland Estates uliopo Mbeya pamoja na hosteli na usafiri wa kisasa.

Katika ligi hiyo Gwambina imepoteza michezo miwili iliyolala mbele ya Geita Gold 1-0, kisha 2-0 katika Uwanja wa Mkwakwani mbele ya Sahare All Stars wakati Namungo FC ilipoteza mchezo mmoja dhidi ya Dar City 2-1.

Rekodi nyingine inayosaka timu hiyo ni ile ya kutoruhusu mabao mengi, kwani hadi sasa imefungwa 12 na kufunga mabao 29, wakati Namungo iliruhusu mabao 14 na kufunga mabao 56.

Wanachosema makocha

Kocha wa timu hiyo, Novatus Fulgence anasema wanachokitazama ni kuhakikisha wanashinda michezo iliyo mbele yao ili msimu ujao wacheze Ligi Kuu.

Michezo iliyosalia kwa timu hiyo katika viwanja vya ugenini ni dhidi Transit Camp, Pamba FC kisha itarejea nyumbani kufunga msimu dhidi ya Rhino Rangers kisha Mashujaa FC.

Kocha wa Ihefu FC, Maka Malwisa alisema kikubwa kwa kocha yeyote ni kuona timu yake inafikisha malengo waliyojiwekea.

“Suala la kuvunja rekodi ni jambo zuri lakini kabla ya kuangalia hayo yote inakupasa kufikia malengo yako, hilo linakuwa muhimu kuliko kitu chochote,” alisema Malwisa.

Rashid Iddi ‘Chama’, kocha aliyekuwa akikinoa kikosi cha Mashuja FC msimu uliopita, alisema Ligi Daraja la Kwanza ni ngumu ndio maana hakuna mfumo maalumu wa timu na jambo la kuweka rekodi linategemea na wachezaji waliopo kwenye timu pamoja na wapinzani unaokabiliana nao.

Kwa sasa Ligi Daraja la Kwanza na zingine zote zimesimama kupisha juhudi za Serikali kukabiliana na janga la corona.