Gor Mahia iko kazi aisee!

Muktasari:

Mabingwa mara 17, wa KPL, Klabu ya Gor Mahia, wataanzia nyumbani kati ya Novemba 27-28, kuwa wenyeji wa Nyasa Big Bullets, ugani Moi Kasarani, Jijini Nairobi, kabla ya kusafiri kuwafuata Wamalawi hao nyumbani kwao, kati ya Desemba 4-5, mwaka huu.

Nairobi. Mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL), Klabu ya Gor Mahia watakuwa na kibarua kigumu katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, msimu wa 2018/19, huku Kariobangi Sharks, wakipangiwa kukutana na Solar7 ya Djibouti.
Kwa mujibu wa ratiba ya michuano ya mechi za mtoano ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Kombe la Shirikisho, iliyotolewa leo Ijumaa, Novemba 9, na Shirikisho la soka Barani Afrika (CAF), ni kwamba watakutana na mabingwa soka nchini Malawi, Nyasa Big Bullets.
Mabingwa hao mara 17, wa KPL, wataanzia nyumbani ambapo kati ya Novemba 27-28, watakuwa wenyeji wa Nyasa Big Bullets, ugani Moi Kasarani, Jijini Nairobi, kabla ya kusafiri kuwafuata Wamalawi hao nyumbani kwao, kati ya Desemba 4-5, mwaka huu.
Ratiba ya michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho ilipaswa kutoka Novemba 3, mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa kamati ya mashindano ya CAF, iliyofanyika Jijini Rabat, Morocco, lakini haikuwa hivyo.
Hali hiyo ilitokana na mabadiliko ya uendeshaji ya michuano inayoratibiwa na CAF, ambayo imepangwa kuendana na ratiba ya ligi nyingine kubwa duniani, kama ilivyoelekezwa na Shirikisho la soka Duniani (FIFA).
Kama watafanikiwa kuwang'oa Nyasa Big Bullets, Gor Mahia watakutana na mshindi wa mechi kati ya UMS de Loum ya Cameroon na Lobi Stars ya Nigeria, katika hatua ya makundi ya michuano hiyo.

BIG BULLETS NI NANI?
Wapinzani wa Gor Mahia, Klabu ya Nyasa Big Bullets, ambao ni klabu yenye mafanikio makubwa nchini Malawi, wakiwa wamechukua ubingwa ligi ya nchini mwa mara 12, wamerejea kwenye Ligi ya Mabingwa Africa baada ya kukosekana kwa zaidi ya miaka mitatatu.
Mara ya mwisho kushiriki michuano hiyo, ilikuwa mwaka 2015, ambapo Nyasa Big Bullets, maarufu kama Bakili Bullets au Bata Bullets, walitupwa nje ya michuano hiyo katika hatua ya mtoano na miamba ya soka nchini Sudan Kusini, Al Hilal. Wanaongoza msimamo wa ligi kuu ya Malawi, huku zikiwa zimesalia mechi mbili tu, watangazwe mabingwa.

KARIOBANGI SHARKS
Wakati mabingwa wa KPL wakipangiwa kuana na Wamalawi, wawakilishi wa Kenya katika mechi za Kombe la Shirikisho, Katriobangi Sharks, ambao walijipatia nafasi ya kushiriki michuano hiyo kwa mara ya kwanza, wamepangwa kuwavaa Solar7 ya Djibouti.
Hii ni ratiba rahisi kwa wakali hao mtaa wa Kariobangi Jijini Nairobi, ikizingatiwa kuwa hawajawahi shiriki michuano hiyo hata mara moja. Bado haifahamiki walifanikiwi vipi kupata tiketi ya kufuzu Ligi ya Mabingwa kwani, msimu uliopita walimaliza katika nafasi ya saba kwenye ligi yao yenye timu 10.
Kama Kariobangi Sharks, itafanikiwa kuvuka hatua hii, watakutana na mshindi wa mechi kati ya Asante Kotoko na timu nyingine ambayo haijajulikana kutoka Cameroon.