MAONI: Fursa ya uenyeji wa Fainali za Afcon U17 isichezewe

INGAWA inawezwa kusemwa kwa sasa ni mapema, lakini ukweli ni kwamba kwa mtu mgeni kutoka nje ya nchi ambaye ni shabiki wa soka hawezi kubaini wala kudhani kama Tanzania ndio watakaokuwa wenyeji wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Vijana U17.

Taifa limebahatika kupewa uenyeji wa fainali hizo za Afcon-U17 kwa 2019 zitakazofanyika kati ya Aprili 14-28, lakini hakuna yale mashamshamu na viashiria vya kuwafanya Watanzania wajiandae kufanikisha fainali hizo, licha ya kusaliwa na mwezi mmoja na ushei tu kabla ya kufanyika kwake.

Huko mitaani hakuna dalili za kufanyika kwa fainali hizo kwa kukosekana matangazo hata ya mabango tu ya kuonyesha mwaka huu sisi ndio wenyeji wa fainali hizo ambazo zitatoa timu wawakilishi wa Afrika katika ushiriki wa Fainali za Kombe la Dunia U17 mwa mwaka huu.

Fainali hizo za dunia zinatarajiwa kufanyikia Peru na kama Tanzania itafanya vizuri inaweza kuandikisha rekodi kwa mara ya kwanza baada ya kuzikosa fainali zilizopita za 2017 zilizofanyika India kutokana na kukwama kuitinga nusu fainali za Afcon U17 zilizofanyikia Gabon mwaka huo.

Kwa jinsi mambo yalivyolala kwa sasa pengine hata mitaani baadhi ya mashabiki hawajui kama ulifanyika uzinduzi wa ‘mascot’ ya michuano hiyo kwa vile tukio hilo halikupewa kipaumbele kikubwa, sio na vyombo vya habari, bali hata na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

TFF haikulifanya kama tukio hilo ni maalum na kulitengeneza kimadoidoi kuhabarisha umma kwamba mambo ndio yameanza kuelekea fainali hizo za Aprili.

Hata baadhi ya vyombo vya habari wamelichukulia poa tukio hilo na maisha yanaendelea kwa kuwa TFF yenyewe imelazimisha hali iwe hivyo.

Hata hivyo kwa kuwa bado tunao muda wa kujipanga, tunadhani mambo yaanze sasa ili kuweka mambo sawa badala ya kusubiri kuwashtukiza mashabiki kuwa sisi ndiop wenyeji wa Afcon 2019.

Na kwa vile hizi ni fainali za kwanza kubwa kwa Tanzania kuandaa ilipaswa kuwe na utofauti, Kitendo cha Habari na kile cha Masoko wangekuwa na kazi moja ya kuanza kutengeneza aina fulani ya mzuka kwa mashabiki mapema ili fainali zikifika hiyo Aprili mambo yawe moto.

Tulitarajia kuanzia sasa kuwepo na mabango na matangazo kuzitangaza fainali hizo kama njia ya kuongeza ushawishi kwa makampuni, wawekezaji na wahisani wengine kujitosa kuzipiga tafu fainali hizo kwa nchi wenyeji na hasa timu yetu ya Serengeti Boys.

Fainali hizi kama wenyeji zimetofautiana kabisa na zile zilizopita wakati Tanzania ilipokata tiketi ya kwenda Gabon. Katika ushiriki ule kulikuwa na kwani mashamshamu yalikuwa mengi na hata timu iliandaliwa vyema ndani na nje ya nchi kwa kupelekwa kambini ng’ambo na hatimaye kushiriki kibabe pale Gabon licha ya kushindwa kutinga nusu fainali kama ilivyotazamiwa.

Tunadhani imefika wakati sasa kitendo cha habari na masoko cha TFF ikishirikiana na Kamati ya Fainali hizo kuchangamkia muda uliosalia kuzitangaza fainali hizo ili zilete tija ikizingatiwa kuwa zinawaletea watu wa mataifa mbalimbali na ni fursa ya kujitangaza kitalii na kujiinua kiuchumi.

Kinywaji cha Coca Cola licha ya kuasisiwa miaka mingi iliyopita na kufahamika zaidi miongoni mwa vinywaji laini, lakini kila uchao kina matangazo mapya na yenye kuhamasisha kunyweka, hivyo tusiachezee fursa tuliyonayo kuelekea fainali hizo za Afrika za Vijana U17.

Tusisubiri dakika za mwishoni kukurukupuka kuzitangaza wakati tuna muda mzuri wa kufanya jambo hilo kwa nafasi na wasaa ili kufanikisha fainali hizo kusudi hata miaka mingine ijayo tukiomba tena Shirikisho la Soka Afrika (CAF) na hata la Dunia (Fifa) liwe radhi kutupa uenyeji wa michuano yoyote mikubwa kwa kujua kutakuwa na ufanisi.

Bado tuna muda, lakini kama nchi tusifanye uzembe fainali hizi zikaondoka bila kutuachia chochote cha kujivunia ndio maana tunakumbusha mambo yaanze sasa kutengenezwa ili yawe moto kwelikweli hata wageni watakaporudi kwao wawe na hamu ya kurudi Tanzania.

Hii ni nafasi hadhimu na haipaswi kuchezewa kwani tukijitangaza vyema na kufanya fainali hizo zifane ni akiba kwetu kwa miaka mingine ijayo.

Shime TFF, serikali na wadau wengine kuhakikisha fainali za Afcon U17 zinakuwa spesho zikijitofautisha na nyingine zilizowahi kufanyika katika mataifa mengine ikizingatiwa kuwa Tanzania kuwa wanaochizika na soka, kwani tujibane wenyewe na fursa ipo mbele yetu.

Tuamkeni sasa!