Ferdinand, Keown wampa somo Arteta

Muktasari:

Mabeki nguli wa zamani England, Rio Ferdinand na Martin Keown wamemtaka kocha wa Arsenal, Mikel Arteta kusajili mabeki bora wa kati, vinginevyo timu hiyo itaendelea kupoteza mechi.

London, England.  Rio Ferdinand, Martin Keown na Joe Cole wamesema kocha Mikel Arteta hana beki wa kati imara katika kikosi cha Arsenal.

Wachambuzi hao walisema Arteta ana bahati mbaya kupata mabeki wa kati dhaifu ambao wamekuwa wakiigharimu Arsenal katika mechi zake.

Kauli za nguli hao wa zamani wa England, zimekuja muda mfupi baada ya mabeki David Luiz na Shkodran Mustafi kufanya uzembe  katika mchezo wa jana usiku ambao Arsenal ilitoka sare ya mabao 2-2 dhidi ya Chelsea.

Wakati Luiz alipewa kadi nyekundu ya moja kwa moja kwa mchezo mbaya, Mustafi alifanya makosa ya mara kwa mara.

Faulo ya Luiz iliipa penalti Chelsea na makosa ya Mustafi kwa kurudisha pasi ya nyuma vibaya yalitoa nafasi kwa Tammy Abraham kuwahi  mpira huo.

“Tunapomzungumzia beki kama Mustafi  kabla ya mechi,  nilikuwa nina hofu kwa mchezaji huyu kama anaweza kucheza kwa kiwango kinachostahili,”alisema Keown.

Keown aliyecheza kwa mafanikio nafasi ya beki wa kati Arsenal, alisema timu hiyo inahitaji beki imara wa kati tofauti na Luiz au Mustafi.

“Ukiwa na mabeki kama Luiz au Mustafi huwezi kuwa na uhakika wa kushinda mechi, itachukua muda mrefu kupata matokeo,”alisema Cole.

Ferdinand alisema Arteta anafanya makosa kumpa jukumu Mustafi kucheza beki wa kati kwa kuwa hana uwezo.