Fei Toto amvuruga kocha Mkongo

Muktasari:

  • Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera amefichua siri kubwa ya kiungo wake Fei Toto kwamba bado kuna madini ambayo Watanzania hawajaanza kuyaona ambayo yatakuwa faida kwa taifa lake.

KAMA unadhani Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliivuruga Cape Verde tu, pole yako kwani kiungo huyo amemvuruga mpaka kocha wake, Mwinyi Zahera ambaye amekiri hajaona kiungo fundi nchini kama nyota wake huyo.

Kocha Zahera alisema hakuna kiungo anayefikia uwezo wa Fei Toto kwa nafasi zote za viungo.

Kauli ya Zahera imekuja siku chache baada ya kiungo huyo kuonyesha uwezo mkubwa katika mchezo wa Taifa Stars dhidi ya Cape Verde mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ambapo Stars waliibuka na ushindi wa bao 2-0.

Akizungumza na Mwanaspoti, Zahera alisema Fei Toto pamoja na umri wake kuwa mdogo anamudu presha za mashabiki na kuonyesha uwezo wa kuisaidia timu kuipa matokeo mazuri jambo ambalo ni nadra kwa vijana kufanya hivyo katika klabu kubwa.

“Ni kijana mdogo sana, ana uwezo mkubwa kutokana na umri alionao anaweza kufika mbali zaidi ya hapo alipo sasa nina muda mchache na nimefuatilia baadhi ya michezo nimegundua Fei Toto ni kiungo bora zaidi Tanzania na akiangaliwa kwa upana anaweza kuwa na msaada kwa taifa lake,”

“Feisal nimekuwa nikimtumia kama kiungo namba sita mara nyingi sana katika kikosi changu sina maana kwamba sitambui kama hana uwezo wa kucheza namba nane hapana namba zote anazimudu kucheza, bado kuna vitu vingi nitaendelea kuvifanyia kazi na atakuwa lulu mbele ya taifa lake,”alisema.

Akizungumzia mchezo wao na Alliance, Zahera alisema anamshukuru Mungu amerudi salama na ameungana na timu ambapo ameikuta iko kwenye hali nzuri na kuweka wazi kuwa wachezaji wake wako fiti na tayari kwaajili ya mchezo huo.

“Tunaingia uwanjani kupambana hatujawabeza Alliance tunawaheshimu kama zilivyo timu nyingine kikubwa tunachotaka kukifanya leo ‘Jana Alhamis usiku’ tutaangalia baadhi ya michezo waliyocheza ili kusoma upungufu wao na ubora wao kabla ya kukutana nao na leo mazoezini kutafanyia kazi,” “Hatudharau timu yoyote inayoshiriki ligi zote ni timu kubwa tutahakikisha tunapambana nia ni kufikia lengo la kushinda mechi zote za nyumbani.