Fedha za Okwi ilivyowatia matatani vigogo wa Simba

Dar Es Salaam. Upande wa mashtaka katika kesi ya vigogo wa klabu ya Simba umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jinsi yalivyofanyika matumizi mabaya ya fedha za mauzo ya mshambuliaji, Emmanuel Okwi kwa klabu ya Etoile Sportive Du Sahel ya Tunisia.

Katika kesi hiyo Rais wa Simba, Evans Aveva na Makamu wake Geofrey Nyange ‘Kaburu’ wanakabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya madaraka, kughushi na kutakatisha fedha.

Katika mashtaka hayayowahusu Aveva na Nyange, yanayohusiana na uhamishaji wa fedha za malipo ya mauzo ya Okwi kutoka akaunti ya klanu kwenda akaunti binafsi ya Aveva.

Mashtaka yao mengine ni kula njama kughushinyaraka, kuwasilisha nyataka za uwongo, kujipatia fedha isivyohalali linalomhusu Aveva peke yake na utakatishajo fedha linalowahusu Aveva na Kaburu.

Mwenyekiti wa Kamati ya usajili, Zacharia Hans Poppe anahusika katika mashtaka mawili ya kughushi na kuwasilisha nyataka za uongo.

Leo Ijumaa Oktoba 19, 2018, kesi hiyo imeanza kusikilizwa katika hatua ya awali ambapo upande wa mashtaka umewasomea washtakiwa maelezo.

Katika maelezo hayo upande wa mashtaka umeeleza jinsi viongozi hao walivyohamisha fedha hizo kutoka akaunti ya klabu kwenda akaunti ya Aveva kwa madai ya kumlipa deni na pia umebainisha jinsi walivyozitumia pesa hizo na namna walivyokwepa kodi.

Akiwasomea maelezo ya awali (PH) Wakili wa Serikali Mwandamizi Shadrack Kimaro akisaidiana na Mutalemwa Kishenyi, alidai kuwa Machi 12, 2016, Klabu ya Simba ililipwa jumla ya Dola za kimarekani 319, 212 na Klabu ya Etoile Sportive Du Sahel ya Tunisia.

Kimaro alidai kiasi hicho cha fedha kilikuwa ni ada ya uhamisho wa mchezaji Emmanuel Okwi kwenda Klabu ya Etoile Sportive Du Sahel.

"Fedha hizo ziliingizwa katika akaunti ya Klabu ya Simba kupitia akaunti namba O1J1026761800 iliyopo katika Benki ya CRDB tawi la Azikiwe.

Amedai kuwa fomu hiyo ya kuhamisha fedha ilisainiwa na mshtakiwa wa kwanza na wa pili ambao ni Aveva na Nyange na maelezo ya malipo katika fomu hiyo, yalikuwa yanasomeka kama malipo ya mkopo.

Kimaro aliendelea kudai kuwa uhamisho wa fedha hizo haukuwa umeidhinishwa na Kamati ya Utendaji ya Klabu ya Simba ilikuwa haijawahi kukopa kiasi hicho cha fedha kutoka kwa mshtakiwa wa kwanza (Aveva).

Amebainisha kuwa, Aveva na Nyange ndio waliokuwa watiaji saini wa akaunti hiyo.

Kimaro aliendelea kudai kuwa baada ya malipo hayo, Machi 15, 2016 kiasi hicho cha Dola 300,000 kilihamishwa kwenda akaunti namba 147002211 ya benki ya Barclays iliyopo tawi la Ohio.

Ameeleza kuwa akaunti hiyo iliyokuwa katika Benki ya Barclays ni akaunti binafsi ya Aveva, ambayo yeye pekee ndio mtiaji saini.

"Uhamisho wa fedha hizo kwenda katika akaunti binafsi ya Aveva, ulitumia fomu ya kuhamisha fedha ya Machi 15, 2016, ambayo iliwasilishwa benki ya CRDB na Aveva.

Alibainisha kuwa kati ya Dola za kimarekani 300,000 zilizoingizwa katika akaunti ya Aveva, mshtakiwa huyo alihamisha Dola za kimarekani 62,183 kwenda kampuni ya Ninah Ghuanzhour Trading Co Ltd.

Akibainisha kuwa pesa hizo zilikuwa kama gharama ya kununua nyasi bandia kwa ajili ya uwanja wa michezo wa Klabu ya Simba, uliopo Bunju wilaya ya Kinondoni.

Aliendelea kudai kuwa kiasi kingine cha fedha ambazo ni Dola za kimarekani 50,000, zililipwa kwa Franklin Lauwo kama gharama za ujenzi wa uwanja wa klabu Simba.

Lauwo ni mmiliki wa Kampuni ya Ranky Infrastructure & Engineering Ltd.

Kimaro alidai mshtakiwa wa tatu katika kesi hiyo, Hanspoppe yeye alikodi Kampuni ya Ranky Infrastructure & Engineering Ltd kufanya Ujenzi wa uwanja huo wakati akijua kuwa kampuni hiyo ilikuwa haujasajiliwa na Bodi ya Wahandisi na Wakandarasi (CRB).

Pia, Hanspoppe anawajibika katika kufanya mchakato wa ununuzi wa nyasi bandia.

Kimaro alidai kuwa bila kujali matumizi kwa baadhi ya pesa hizo kwa ununuzi wa nyasi bandia na uhusika wa kampuni ya Rank hiyo, Aveva na Kaburu hawakuweza kutoa maelezo ya Dola za Marekani 187,817 ambazo ziliingizwa kwenye akaunti ya Aveva.

Kimaro alidai kuwa kwa ajili ya kuondoa nyasi bandia zilizokuwa zimeingizwa katika Bandari ya Dar es Salaam, Aveva, Nyange na Hanspoppe walitengeneza hati ya malipo ya uongo namba 201605280001 na kuiwasilisha Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), 

Amebainisha kuwa hati hiyo ilikuwa inaonyesha thamani ya Nyasi bandia ilikuwa Dola za kimarekani 40,577 na kwamba hati hiyo ilitengenezwa kwa lengo la kukwepa kodi.

Kesi imeahirishwa hadi hadi Oktoba 31, ambapo upande wa mashtaka unaanza kutoa ushahidi.