FEDERER: Jamaa ana hela hadi anakera

MELBOURNE, AUSTRALIA. KUITWA bilionea si jambo dogo ujue. Hilo jina linaenda kwa watu wenye pesa kwelikweli si ungaunga mwana.

Unaambiwa licha ya kupiga pesa ndefu kwenye matangazo na mishahara, lakini wanamichezo watatu tu ndiyo wana mkwanja wa kutosha kiasi cha kuitwa mabilionea.

Floyd Mayweather, Michael Jordan na Tiger Woods ndiyo wanamichezo wenye pesa ya kutosha kiasi cha kufikia hadhi ya ubilionea.

Lakini, katika mwaka 2020 hii orodha ya mabilionea katika michezo itaongezeka kwa sababu gwiji wa tenesi, Roger Federer anatarajiwa kuingia katika listi hii.

Federer anatarajiwa kuwa mwanamichezo bilionea wa nne kutokana na dili za pesa zilizopo mbele yake kwa mwaka huu wa 2020, ambazo zinatazamiwa kuongeza kipato chake maradufu.

Federer anavyopiga pesa

Pesa za Federer zinatokana na zawadi za mataji aliyoshinda pamoja na matangazo na udhamini wa kampuni kibao kubwa duniani.

Hadi sasa Federer anakadiriwa na kipato cha Pauni 689 milioni, huku Pauni 153 milioni nyingine zikitarajiwa kuingia mwaka huu kutokana na mikataba yake ya matangazo.

Kutokana na zawadi za mashindano aliyoshiriki na kushinda Federer ameingiza jumla ya Pauni 98 milioni. Kila mwaka huingiza Pauni 7.6 milioni kwa kushiriki tu michuano ya kujiandaa na msimu ya Amerika Kusini.

Lakini, inadaiwa kuwa ni biashara na matangazo yake ndiyo vinamuingizia kipato kikubwa zaidi gwiji huyo wa tenesi mwenye umri wa miaka 38.

Federer ana mikataba mikubwa ya udhamini na Kampuni za Rolex, Uniqlo, Credit Suisse na Mercedes Benz, Rimowa, Moet & Chandon na Barilla kupitia kampuni hizi kwa mwaka Federer anaingiza zaidi ya Pauni 80 milioni.

Mwaka 2018, Federer aliingia mkataba wa miaka mitatu na Kampuni ya Uniqlo wenye thamani ya Pauni 23 milioni kwa mwaka, lakini pia, Federer ana mkataba mnono na Kampuni ya Viatu ya Nike, huku mwenyewe akiwa na kiwanda cha viatu viitwavyo ON.

Mfuko wake wa kusaidia jamii umezalisha zaidi ya Pauni 30.7 milioni na zimetumika kusomesha watoto milioni 1 wanaoishi katika mazingira magumu barani Afrika.

Familia na makazi

Mwaka 2009, Federer alimuoa mchezaji wa zamani wa tenesi, Mirka Vavrinec, Julai mwaka huo wawili hao walifanikiwa kupata watoto mapacha wa kike, Myla na Charlene. Mei 6, 2014, wawili hao walipata watoto wengine mapacha lakini safari hii walikuwa wa kiume Leo na Lenny. Federer na familia yake wanaishi Bottmingen, Uswiss.

Staa huyo ana bonge la mjengo kwenye fukwe za Ziwa Zurich. Mbali na mjengo huo Federer ana nyumba nyingine mbili moja ni ya mapumziko iko nchini Uswiss ikiwa na thamani ya Pauni 13 milioni, wakati nyingine ni apatiment iko kwenye ghorofa la Le Reve, Dubai.

Matumizi

Ukiwa na pesa lazima ujue kuzitumia, mwaka 2003, Federer alianzisha mfuko wake wa kusaidia Jamii wa Roger Federer Foundation, kwa kuanzia aliweka Pauni 21.8 milioni kwa ajili ya kusapoti elimu kwenye Bara la Afrika na Uswiss

Lakini, mbali na kutumia fedha katika kusaidia watu wasiojiweza, Federer ni mpenzi sana wa fasheni na mwenyewe anasema pesa yake nyingi anatumia kununua nguo kwa sababu hapendi kutoka akiwa hajapendeza.

Mbali na nguo Federer anamiliki saa ya Rolex Sky Dweller yenye thamani ya Pauni 30,734 na pia ana magari sita aina ya Mercedes Benz, ndege binafsi na boti ya kifahari.

Ni nani?

Federer alizaliwa Agosti 8, 1981, Uswiss sasa anashika nafasi ya tatu kwa ubora wa tenesi duniani, anashikiria rekodi ya kutwaa mataji mengi zaidi ya Grand Slam akifanya hivyo mata 20. Alianza kucheza tenesi ya kulipwa mwaka 1998, na tangu wakati huo amekuwa moto wa kuotea mbali.