FDL kuisha kibabe, Dodoma, Ihefu kitaeleweka

Friday July 10 2020

 

By YOHANA CHALLE

LIGI Daraja la Kwanza (FDL) inamalizika kesho Jumamosi kwa kushuhudia viwanja 11 vikiwaka moto baada ya juzi kuishuhudia Sahare All Stars ikishushwa daraja kwa kichapo cha mabao 2-0 dhidi ya Arusha AFC.

Tayari Gwambina imekata tiketi ya kucheza Ligi Kuu msimu ujao huku Geita Gold nayo nikijihakikishia kucheza hatua ya mtoano, lakini Kundi A linaloongozwa na Dodoma Jiji yenye alama 48 sawa na Ihefu watangoja hatma yao katika michezo ya kesho Jumamosi.

Dodoma itakuwa nyumbani Uwanja wa Jamhuri, kucheza na Iringa United ambayo nayo inasaka alama tatu ili kukwepa kushuka daraja wakati Ihefu ikiikaribisha Cosmopolitan ambayo tayari imeaga ligi hiyo.

Michezo mingine ya kesho Jumamosi Kundi A, Njombe Mji na Mbeya Kwanza, Boma FC na Friends Rangers, Pan African na Majimaji, African Lyon dhidi ya Mlale FC.
Kundi B, Gwambina atacheza na Mashujaa, Pamba dhidi ya Rhino Rangers, Mawenzi Market na Stand United, Geita Gold na Transit Camp wakati Gipco akicheza na Green Warriors.

FDL ilianza kutimua vumbi Septemba 14 mwaka jana na sasa inafikia tamati huku moja ya vitu vitakavyokumbukwa msimu huu ni namna ushindani wa timu ulivyokuwa.

Matokeo ya mzunguko wa kwanza yalikuwa hivi: Boma FC iliicha 1- 0 Mlale FC, Sahare All Stars ilishinda 3-1 mbele ya Trans Camp, Dodoma Jiji FC ilivuna alama tatu mbele ya Cosmopolitan iliposhinda 2 -0, Ihefu FC iliifunga 2-0 Majimaji FC.

Njombe Mji ikiwa nyumbani ilishinda 1-0 mbele ya Friends Rangers, Geita ilibanwa mbavu ya mabao 2-2 dhidi ya Mashujaa, Gwambina FC ikiichapa 3-0 AFC, Iringa United ilipoteza 2-0 mbele ya Africans Lyon, GIPCO ikachapwa 1-2 dhidi ya Rhino Rangers.

Green Warriors ilitoa suluhu mbele ya Mawenzi, Pamba FC ikaichapa 3-1 Stand United, Pan African ilichapwa 1-3 na Mbeya Kwanza.

Advertisement