Eymael ajipanga kivingine

NI mwanzo mbaya na mgumu kwa kocha mpya wa Yanga, Luc Eymael akipoteza michezo miwili muhimu mbele ya mashabiki wa klabu hiyo kwenye viwanja viwili maarufu jijini Dar es Salaam; Uhuru na Taifa.

Ni matokeo ambayo yamewanyima furaha mashabiki wa timu hiyo na mara ya mwisho walikuwa na mzuka mwingi wakipindua meza kibabe pale Uwanja wa Taifa kwa kutoka nyuma kwa mabao 2-0 na kurudisha yote dhidi Simba.

Baada ya hapo, mashabiki wa Yanga walitoka vichwa chini kwenye mechi dhidi ya Kagera Sugar wakichapwa mabao 3-0 kisha juzi wakapigwa tena na Azam FC kwa bao 1-0. Matokeo hayo yameanza kumuumiza kichwa Eymael ambaye amefichua kwamba hafahamu hatima yake na kikosi chake, lakini atakutana na kamati yake ili kuangalia mambo sahihi ya kufanya.

Akizungumza na Mwanaspoti baada ya mchezo wao na Azam FC, Eymael alisema kwa matokeo hayo ni lazima akae chini na kuanza kufikiria maisha yake siku zijazo kwa kukaa na viongozi wa klabu yake.

Alisema kuwa amezoea kushinda na kubeba mataji, lakini matokeo katika mechi zake mbili yanamnyima usingizi.

“Nimezowea kushinda mataji katika nchi ambazo nimepita kufundisha, mambo yanayoendelea hapa sifurahishwi nayo, hivyo nitakaa na kamati yangu kuona itakuwaje,” alisema Eymael raia wa Ubelgiji.

“Tumecheza mechi mbili lakini hatujapata pointi hata moja katika sita, hivyo lazima mwenyewe nijiangalie kuhusu kesho yangu.”

Pia alisema yeye ni muumini wa falsafa ya kutumia mfumo wa mshambuliaji mmoja, lakini timu yake ya ufundi inapendelea zaidi washambuliaji wawili.

“Najua hapa wote mnapenda mfumo wa washambuliaji wawili mbele, hata uongozi wangu unapenda hivyo. Lakini, tulianza na mshambuliaji mmoja kipindi cha kwanza na cha pili nililazimika kumuingiza mshambuliaji wa pili, vipi kuna tofauti ambayo imeonekana?” alihoji Eymael, ambaye alionekana kutofurahishwa. Kuhusu kutopata goli kupitia kwa washambuliaji wake, Eymael alisema wamekuwa wakitengeneza nafasi nyingi lakini inaonekana hawana bahati.

Humwambii kitu kwa Molinga

Kama ilivyodokezwa kwenye toleo la Mwanaspoti Jumamosi, ambapo Eymael aliwagomea mabosi wake kumtema straika David Molinga kisha akaahidi kuwa atamtumia kwenye mchezo na Azam FC, Eymael juzi alimuanzisha kwenye kikosi cha kwanza akicheza kwa dakika zote 90.

Jana tena Eymael akafunguka kuwa hakujutia uamuzi wa kumrudisha Molinga katika timu kwani licha ya kufanya mazoezi mepesi kwa siku mbili, alionyesha kiwango bora dhidi ya Azam.

“Kwa washambuliaji, Molinga anaweza kufunga mabao mengi zaidi kama atapata muda wa kutosha uwanjani na kufanya mazoezi ya pamoja na wenzake.”

WAILALAMIKIA BODI

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu wa Yanga, Dk. David Ruhago ameilalamikia Bodi ya Ligi kwa kubadilisha ratiba mara kwa mara hasa mchezo wao dhidi ya Singida United.

Alisema mechi na Singida United, awali ilipangwa kuchezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha na Yanga imeshakamilisha taratibu zote za kuweka kambi jijini humo ikiwemo usafiri na hoteli. Hata hivyo, mchezo huo umebadilishwa na sasa utapigwa Singida.