Eymael: Huo mziki hapo mbele Mtajuta

KOCHA Mkuu wa Yanga, Luc Eymael amesema kama hesabu zake zote zikitiki huo mziki anaoshusha hapo kwenye safu ya ushambuliaji kuna watu watatafutana.

Eymael ametamba kwa kujiamini kwamba, akili yake kwa sasa ipo kwenye ushambuliaji na winga zote mbili katika usajili mpya.

Na tayari ameshamalizana na baadhi ya wachezaji na anashukuru kwamba, uongozi chini ya udhamini wa GSM wanakwenda kasi katika kuhakikisha mapendekezo ya wataalamu wa benchi la ufundi yanafanyiwa kazi.

Akizungumza na Mwanaspoti moja kwa moja kutoka Ubelgiji alipo kwa sasa, Eymael alisema anataka timu yenye kasi na watu wa kazi ambayo hata straika aina ya Bernard Morrison awe anasota kupata namba kwenye kikosi cha kwanza.

Pia, amesema hata mchezaji anapokosekana kikosi basi hakuna pengo kutokana na waliopo kuwa na uwezo wa kuziba nafasi hiyo na mashabiki wanafurahi.

Alisema anamhitaji pia kiraka Mbelgiji, Andrea Fileccia anayechezea klabu ya ridhaa ya daraja la kwanza nchini humo ya Royal Francs Borains.

“Nataka kuwa na wigo mpana hasa kule mbele, yaani aliyeko ndani na aliyeko benchi wote wawe na ubora stahiki wenye hadhi ya kuichezea Yanga.

“Huyu Andrea ni kama Morrison makali yake, lakini yeye ana uwezo wa kucheza hadi nafasi ya mshambuliaji wa kati. Huyu sehemu ni Morrison na sehemu ni Nchimbi,” alisema akimaanisha kwamba, anaweza kucheza pembeni na katikati, ana asisti na kufunga.

Eymael alisema akipata saini za mastraika na mawinga wa kigeni kutoka DR Congo, Ghana na Rwanda aliowapendekeza pamoja na wale wazawa, basi Yanga itakuwa moto kwelikweli.

Kocha huyo anataka angalau kila nafasi ndani ya kikosi cha kwanza iwe na wakali wawili mmoja wa kigeni na mwingine mzawa, akianza mmoja mwingine awe akipasha pembeni ili kuongeza ushindani.

Mpaka sasa Yanga ina uhakika wa kuwapa mastaa wawili kutoka DR Congo kwenye ushambuliaji ambao ni Tuisila Kishinda wa AS Vita na Mpiana Mozizi wa FC Lupopo.

KUHUSU ANDRE

“Namjua sana kwani mbali ya kucheza hapa Ubelgiji, pia alicheza Afrika Kusini katika klabu zinazoshiriki Ligi Kuu kama Free State Stars kuanzia mwaka 2014 mpaka 2016 na Maritzburg United kuanzia mwaka 2016 mpaka mwaka jana kabla ya kujiunga na kurejea nchini mwaka jana.”

“Ni mchezaji mzuri, ana nidhamu ndani na nje ya uwanja, anajua kuitumikia klabu na vile vile amekuwa msaada mkubwa katika timu alizocheza,” alisema Eymael.

Mbali ya timu hizo, Fileccia pia alicheza timu za vijana za Feyenoord ya Uholanzi. Pia alicheza Ligi Kuu ya Uholanzi akiwa na SBV Excelsior ambayo alichezea kwa mkopo kuanzia mwaka 2010 mpaka 2012 na mechi yake ya kwanza ilikuwa Agosti 7, mwaka 2010 dhidi ya timu ya De Graafschap.

Alisema kuwa Fileccia ni chaguo lake ili kukamilisha safu yake ya ushambuliaji.

“Nikiwa na Morrison (Benard), Nchimbi (Ditram) na wengine wapya, ninataka kuwa na kikosi bora ambacho kitakuwa kinapata matokeo mazuri kila mechi,” alisisitiza Eymael.

Kocha huyo amesisitiza msimu huu wakirejea uwanjani amepanga kuukamilisha kwa heshima ya aina yake kwavile nafasi yao ya ubingwa ni finyu ila akili zao zipo kwenye kombe la FA. Anasema kwamba lazima wabebe FA ili kupata aina ubora wa wachezaji anaotaka kwani wengi kigezo chao cha kusajiliwa ni shauku ya kushiriki mashindano makubwa ya kimataifa.

Fileccia alizaliwa Desemba 6, 1991 ambapo kwa sasa ana miaka 28.