Eymael: Haruna, Morrison? subirini tu mtafurahi

Friday July 10 2020
haruna pic

KUUMIA kwa Haruna Niyonzima katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Biashara United kulizua hofu kwa mashabiki wa Yanga kuelekea pambano la ‘Kariakoo derby’, lakini habari njema zinazomhusu ni kwamba anaweza kukipiga katika mchezo huo wa nusu fainali ya Kombe la FA, Jumapili.

Kocha wa Yanga, Luc Eymael amefichua kwamba kuna zaidi ya asilimia 50 kwa kiungo huyo na beki wake wa kulia, Juma Abdul kuwa sehemu ya mchezo wa Jumapili dhidi ya Simba. “Tutawaangalia mazoezini ndani ya siku hizi chache ambazo zipo mbele yetu, kuna zaidi ya asilimia 50 kuwa nao katika mchezo wa Jumapili, tusubiri kuona kama asilimia hizo zinaweza kuongezeka, ni wachezaji muhimu kwetu,” alisema kocha huyo.

Abdul na Niyonzima hawakutumika katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar ambao Yanga waliibuka na ushindi wa bao 1-0, lililofungwa na Benard Morrison.

Kuhusu kurejea kwa Morrison kikosini, Eymael alisema kumeongeza nguvu na ana imani kuwa makali yake ataendelea kuyaonyesha katika mchezo dhidi ya Simba licha ya sakata lake na mabosi wa Yanga lililotokea siku chache zilizopita na kuzua gumzo kwa mshabiki wa timu hiyo. “Morrison ni mchezaji muhimu ambaye bado tunamhitaji, lakini ni lazima atambue kuwa hakuna mtu au mchezaji mkubwa kuliko klabu, ndio maana nilimuondoa kambini.”

Nyota huyo raia wa Ghana ndiye aliyeiliza Simba katika mchezo wa mwisho kukutana kati ya miamba hiyo ya soka la Tanzania katika mchezo ambao ulichezwa Machi, 2020, ambapo Yanga iliibuka na ushindi wa bao 1-0.

KAMBI YA KAGERA

Advertisement

Yanga wamebakia mkoani Kagera kujiandaa na mechi shidi ya Simba ambapo kwa mujibu wa Makamu Mwenyekiti Fredrick Mwakalebela wamesalia huko kwa kuwa hali ya hewa ni rafiki kwao.

Alisema hawana shaka na mchezo huo na huko Kagera, wanazidi kujiandaa kuelekea katika mchezo huo muhimu kwao.

“Tumebaki Kagera kujiandaa dhidi ya Simba, ni baada ya mchezo wetu na Kagera Sugar. Tutarejea siku moja kabla ya mchezo wetu,” alisema na kuongeza kuwa kama viongozi wanaseti mipango na wanaamini itakuwa sahihi kupandisha zaidi morali ya wachezaji.

Advertisement