Eto'o kuzindua uwanja soka la ufukweni Dar

Muktasari:

  • Eto’o ni Mwafrika wa kwanza kutwaa mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa akiwa na klabu za Barcelona na Inter Milan

Dar es Salaam. Mchezaji nyota wa zamani wa klabu ya Barcelona, Real Madrid, Chelsea na  Inter Milan, Samuel Eto’o atawasiji nchini keshokutwa Jumatano kwa ajili ya kuzindua ujenzi wa uwanja wa mpira wa miguu wa wachezaji watano eneo la Ufukwe wa Oysterbay .

Mbali ya uzinduzi wa ujenzi wa uwanja huo uliofadhiliwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Eto’o kwa sasa anachezea klabu ya Qatar FC pia ataendesha mafunzo ya wachezaji wa  Chipukizi wa Manispaa ya Kinondoni.

Meneja wa Bia ya Castle, Pamela Kikuli alisema ujenzi huo utagharimu Sh400 milioni na uwanja huo utakamilika baada ya miezi nane.

Kikuli alisema kuwa TBL imeamua kujenga uwanja huo kwa kushirikiana na Manispaa ya Kinondoni ikiwa ni kusaidia jamiii kupitia michezo.

“Tumekuwa tukiendesha michezo ya Castle Lager 5-A-Side ambapo washindi wake ushindana katika mashindano ya Afrika na ya kimataifa, tumefarijika kuona mchezo huo unapendwa, lakini hakuna kiwanja rasmi kwa ajili ya mashindano, tumeamua kujenga uwanja huu ikiwa ni mwanzo tu wa uwekezaji wetu katika michezo nchini,” alisema Kikuli.

Kikuli alisema kuwa uwanja huo utatumika kwa jamii kwa utaratibu maalum ambao utawekwa na kampuni yao kwa kushirikiana na Manispaa ya Kinondoni.

Alisema, TBL kupitia bia yake ya Castle Lager imeamua kujenga uwanja huo kama sehemu ya kurudisha fadhila kwa jamii ya watanzania ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikiwaunga mkono kibiashara.

 “Sisi sote huwa na ndoto ya kupata nafasi ya kuwaona wachezaji wa kimataifa, haswa wale wenye majina makubwa kama Eto’o. Castle Lager ina furaha kubwa kufanya ndoto hii kuwa kweli kwetu sote kwa kutuletea Mchezaji huyu mwenye hadhi ya kimataifa hapa nyumbani,” alisema Kikuli.

“Tulifanya mashindano hayo na sasa tumeona kuna umuhimu kuwa na uwanja ambao utatumika bure kwa watanzania katika kukuza vipaji vya mchezo huu, hatimaye tupate wawakilishi wazuri  kimataifa kwa miaka ijayo.  Mashindano haya yanafanyika kila mwaka ambapo Tanzania tumeanza mwaka huu,” alisema Kikuli.

Akizungumza katika hafla hiyo, balozi wa bia ya Castle lager, Ivo Mapunda alisema anaamini uwepo wa Eto’o nchini itakuwa chachu kwa Watanzania kushiriki katika mchezo huo.

Alisema kuwa jitihada ambazo zimekuwa zikifanywa na Castle Lager katika kukuza michezo hazina budi kufuatwa na wadau wengine wa michezo katika kukuza vipaji nchini.

Aliwataka wakaazi wa Dar es Salaam na vitongoji vya jirani kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi huo ambapo watapata fursa ya kupiga picha za kumbukumbu na Eto’o, akisisitiza kuwa nafasi kama hizo hupatikana mara chache.