Eriksen atengewa dili la kijanja Madrid

Muktasari:

  • Ceballos kwa sasa yupo kwenye majukumu ya timu ya taifa akitumikia kikosi cha Hispania cha wachezaji chini ya umri wa miaka 21 na alifunga bao Jumapili iliyopita kwenye mechi ya kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Italia.

MADRID, HISPANIA. REAL Madrid wapo tayari kuwapa Tottenham Hotspur ofa ya Pauni 45 milioni pamoja na kiungo Dani Ceballos ili wao wamchukue Christian Eriksen.
Kocha wa Real Madrid, Zinedine Zidane amemweka kiungo huyo wa Spurs kwenye orodha ya wachezaji wake anaowaka kutoka kwenye Ligi Kuu England baada ya kumnasa supastaa wa Chelsea, Eden Hazard.
Ceballos kwa sasa yupo kwenye majukumu ya timu ya taifa akitumikia kikosi cha Hispania cha wachezaji chini ya umri wa miaka 21 na alifunga bao Jumapili iliyopita kwenye mechi ya kichapo cha mabao 3-1 kutoka kwa Italia.
Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 22 amemwambia kocha Zidane kwamba anataka kuondoka baada ya kukosa nafasi ya kucheza msimu uliopita. Spurs wamekuwa wakihusishwa naye kwa miezi kadhaa sasa, lakini shida ilikuwa pesa tu kwamba Mauricio Pochettino hakupewa.
Lakini, kwa sasa dili hilo linaweza kukamilika kirahisi kutokana na ukweli kwamba Real Madrid wanamtaka Eriksen, hivyo wapo tayari kutoa pesa na mchezaji huyo ili kuwashawishi wababe hao wa London.
Mwenyekiti wa Spurs, Daniel Levy anaamini kwamba kiungo wake Eriksen thamani yake ni Pauni 100 milioni, hivyo kama kuna timu itakayokuwa tayari kulipa kiwango hicho cha pesa itakuwa tayari kuwauzia.