Emery kukimbiza mastaa Arsenal

Muktasari:

Kelele za mashabiki na viongozi wa Arsenal kumtaka Unai Emery kuondoka zimezidi kupamba moto na sasa kuna tishio la wachezaji nyota kutaka kuondoka.

London, England . MAMBO sio mazuri ndani ya Emirates. Mabosi wa Arsenal wameanza kuingiwa hofu na mustakabali wa wachezaji wao nyota kuondoka klabuni hapo kama mambo yataendelea kuwa mabaya na timu kupoteza mechi.
Hofu kubwa kwa sasa ni kwamba, kama Kocha Unai Emery ataendelea kuinoa Arsenal basi kuna hatari wachezaji nyota wakiwemo nahodha, Pierre-Emerick Aubameyang na Alexandre Lacazette hawatasaini dili mpya na wataomba kuondoka.
Habari kubwa kwenye korido za Emirates kwa sasa ni Unai ataondoka lini klabuni hapo na kama ataachwa hadi mwishoni mwa msimu basi msimu ujao kuna wimbi kubwa la wachezaji wataondoka.
Kwa mujibu wa Dailymail inaaminika kwamba, mabosi wa Arsenal Raul Sanllehi na Mkurugenzi wa Michezo, Edu wamekutana na kufanya kikao cha dharura na Unai baada ya sare ya mabao 2-2 dhidi ya Southampton, ambapo mashabiki wa Arsenal walipandwa hasira.
Hata hivyo, habari za ndani zinafichua kuwa tayari mabosi wa Arsenal wameanza mchakato wa kutafuta mrithi wa Unai ikiwa ni mkakati wa muda mrefu kulinda mastaa wasiondoke.
Wachezaji na viongozi kwenye benchi la ufundi wamekuwa wakihoji mbinu za ufundishaji za Unai, ambazo zimekuwa zikiifanya Arsenal kushindwa kupata matokeo mazuri na hofu kubwa kwa sasa ni kushindwa kufuzu kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.