Ed Woodward hapati usingizi kisa nyota hawa

Muktasari:

Hawa hapa nyota watano ambao Ed anapambana kuhakikisha wanatua Manchester United kama si wote, basi hata wawili.

MANCHESTER, ENGLAND . KABLA ya Ligi Kuu England kusimama kwa dharura kutokana na kusambaa kwa virusi vya corona, Manchester United ilikuwa imeshika kasi kufukuzia nafasi nne za juu kwenye msimamo.

Walikuwa wameshinda mechi 10 za mashindano yote, ambapo rekodi inaonyesha kuwa mara ya mwisho kufungwa ilikuwa ni Januari 22. Kutua kwa kiungo fundi wa Ureno, Bruno Fernandes aliyesajiliwa kwenye dirisha la Januari kuliongeza ubora wa kikosi cha Kocha Ole Gunnar Solskjaer.

Hata hivyo, bado bosi kubwa wa wababe hao wa Old Trafford, Ed Woodward hapati usingizi kutokana na kupambana kuwashusha kikosini mastaa ambao anaamini watairejesha Manchester United kwenye enzi zake.

Hawa hapa nyota watano ambao Ed anapambana kuhakikisha wanatua Manchester United kama si wote, basi hata wawili.

JADON SANCHO

Kwenye orodha ya wachezaji wanaotakiwa huko Old Trafford, jina la winga wa Borussia Dortmund ya Bundesliga, Jadon Sancho, lipo. Mwaka 2017 alikuwa mmoja wa makinda hatari kwenye kikosi cha Manchester City.

Pep Guardiola na mabosi wa City walipambana kuhakikisha anabaki Etihad, lakini Sancho alikuwa na mipango mingine na kwenda kutua zake Borussia Dortmund ambako sasa amekuwa staa mkubwa na mwenye thamani kubwa.

Manchester United imejaribu mara kadhaa kwenye dirisha la usajili lililopita, lakini harakati hizo hazikukamilika. Thamani ya Sancho inatajwa kufikia Pauni 120 milioni na Woodward amepania kumshusha Old Trafford.

Hata hivyo, Manchester United itakuwa na shughuli ya kupambana na Chelsea, Liverpool na Arsenal ambazo nazo zinawania huduma ya winga huyo wa Kiingereza.

KALIDOU KOULIBALY

Kabla ya Manchester United kuvunja akaunti na kulipa Pauni 80 milioni kwa Harry Maguire, macho na mipango yote ilikuwa kwa beki wa kati wa Senegal anayekipiga Napoli, Kalidou Koulibaly.

Kwa sasa inaelezwa kuwa kwenye orodha ya mabeki wa kati bora duniani kwa yumo ukiacha Virjil van Dijk wa Liverpool basi anayefuata ni Koulibaly.

Woodward anataka kumleta Msenegali huyo Old Trafford ili kusuka ukuta wa chuma akicheza sambamba na Maguire, Victor Lindelof au Eric Bailly. Hata hivyo, Napoli ambao wanaweza kufikia makubaliano ya kumweka sokoni beki huyo hawatakuwa tayari kuanza mazungumzo bila kuwekwa Pauni 100 milioni mezani.

ERLING HAALAND

Kwenye dirisha dogo la Januari, mwaka huu, Manchester United walipewa nafasi kubwa ya kumsajili kinda wa miaka 19 Erling Haaland. Hata hivyo, mambo yakawa tofauti kabisa na mwisho kukaibuka mgogoro mzito baina ya mabosi wa Man United na wakala Mino Raiola ambaye anamsimamia kinda huyo.

Inaelezwa kuwa Raiola aliweka vipengele vya kumnufaisha zaidi kwenye mkataba wa kinda huyo jambo ambalo Man United hawakukubaliana nalo na kusitisha mpango huo, na Haaland akaelekea zake Signal Iduna Park tena kwa pesa ndogo tu.

Kwa sasa thamani ya Haaland imepanda hadi kufikia Pauni 100 milioni huku wababe kibao wa Ulaya wakiwemo Real Madrid, Barcelona na Liverpool wakifuatilia kwa karibu maendeleo ya kinda huyo aliyeanza kwa kasi ya kupachika mabao.

JAMES MADDISON

Pale Kings Power kuna dogo mmoja anaitwa James Maddison ambaye rada zake zinasoma kuwa kama siyo sasa, basi baadaye atakuwa amevaa jezi ya Manchester United.

Mara kadhaa Man United wamekuwa wakiulizia mkataba wa Maddison, lakini usajili wa hivi karibuni wa Fernandez unaweza kuzima dili hilo.

Hata hivyo, mvutano wa kiungo Paul Pogba wa kutaka kuondoka Old Trafford unaweza kufufua matumaini ya Maddison kukipiga Man United, kwani ni aina ya mchezaji ambaye Ole anataka kuwa nao klabuni kwake.

JACK GREALISH

Nahodha wa Aston Villa ambayo kwa sasa inapambana na hali yake huko chini ya msimamo wa Ligi Kuu England.

Staili ya uchezaji ya Maddison inafanana kabisa na supastaa huyo wa Aston Villa, Jack Grealish.

Viungo hawa wote wanafiti kwenye mfumo wa Ole huku suala la umri mdogo likiwaongezea sifa ya kukipiga Old Trafford.

Jack anapatikana kwa dau la Pauni 60 milioni, na kama Aston Villa itashuka daraja basi kuondoka kwake hakuna mjadala na thamani yake huenda ikashuka zaidi.