Duh! Naomi amgalagaza Serena kwa mkwanja

LONDON ENGLAND. UNA hela? Staa wa kike wa mchezo wa tenisi, Naomi Osaka amempiku mkongwe Serena Williams kwa kuwa mchezaji aliyepiga pesa nyingi zaidi kwa mwaka uliopita, kwa mujibu wa Forbes.

Jarida hilo la kibiashara linaripoti kwamba staa huyo wa tenisi mwenye umri wa miaka 22 kutoka Japan, ameweka kibindoni Pauni 30.7 milioni ndani ya miezi 12 iliyopita kutoka kwenye zawadi na malipo mengine, ikiwani zaidi ya Pauni 1.1 milioni alizovuna Serena.

Kiwango hicho kinazidi pia kile alichovuna Maria Sharapova mwaka 2015 cha Pauni 24.4 milioni kilichokuwa kikiweka rekodi kwamba ni kikubwa zaidi kuwahi kukusanywa na mcheza tenisi wa kike ndani ya mwaka mmoja.

Osaka anashika namba 29 kwenye orodha ya jumla ya wakali waliovuna pesa nyingi ndani ya mwaka mmoja kwa wanamichezo 100, huku Serena akishika namba 33.

Serena, 38, ambaye ni Mmarekani alikuwa akiongoza kwa kuvuna pesa nyingi kwa upande wa wanawake karibu kila mwaka kwa kipindi cha miaka minne iliyopita.

Mwaka 2018, Naomi Osaka alimchapa Serena Williams kwenye mashindano ya US Open na kubeba taji lake la kwanza la Grand Slam la mchezo wa tenisi kwa upande wea wanawake kabla ya kwenda kubeba taji la Australian Open miezi mitano baadaye.

Kwa sasa Naomi Osaka anashika namba 10 katika viwango vya ubora wa mchezo huo wa tenisi kwa upande wa wanawake duniani.