Duh! Luiz kapiga pesa kibao Arsenal

LONDON ENGLAND. BEKI Mbrazili, David Luiz ameigharimu Arsenal mkwanja wa Pauni 24 milioni ndani ya msimu mmoja tu aliotumikia timu hiyo kwenye Ligi Kuu England.

Luiz alisaini mkataba wa mwaka mmoja kwenye siku ya mwisho ya kufungwa kwa dirisha la usajili Agosti mwaka jana na sasa Mbrazili huyo amekiri kwamba anafunguliwa mlango wa kutokea na mwisho wa msimu ataondoka zake.

Lakini, Arsenal wakati wanamsajili, waliwalipa Chelsea mkwaja wa Pauni 8 milioni kwenda kuziba pengo la nahodha wao, Laurent Koscielny.

Kwa mujibu wa The Athletic, kwenye dili hilo, Arsenal walilipa pia Pauni 6 milioni kwa wakala kama kamisheni yake baada ya wakala huyo, Kia Joorabchian kufanya jambo kubwa kwenye kumshawishi Luiz kwenda Arsenal tena kwa pesa ndogo kiasi hicho.

Hata hivyo, mkwanja wa kumgharimia Luiz haukuishia hapo, beki huyo wa kati anaripotiwa kulipwa Pauni 125,000 kwa wiki, huku malipo yote pamoja na bonasi kwa mwaka ikiwa Pauni 10 milioni na hivyo kufanya awe anigharimu Arsenal Pauni 24 milioni ndani ya msimu mmoja tu, ambao hadi sasa amecheza mechi 32 pekee.

Klabu hiyo ilikubali pia kumsainisha mkataba wa muda mfupi kutokana na ligi kushindwa kumalizika kwa wakati huku mchakamchaka huo ukitarajia kuendelea Juni 17, ambapo Arsenal watashuka uwanjani kuwakabili Manchester City.

Luiz, mwenye umri wa miaka 33, kwa sasa anapiga hesabu za kurudi kwenye klabu yake ya zamani ya Benfica, lakini dili hilo kuweza kukamilika, staa huyo itabidi akubali kupungumza mshahara wake.

Tangu ametua Arsenal Luiz amehusika katika makosa kadhaa yaliyoigharimu timu licha ya wakati mwingine kucheza vyema.