Samatta: Taifa Stars kazi bado ipo!

Muktasari:

Baada ya ushindi wa mabao 2-0, dhidi ya Cape Verde, Mbwana Samatta wa Genk amesema, Taifa Stars bado ina kazi kubwa kufanikisha safari ya Cameroon mwakani.
Doris Maliyaga

Dar es Salaam. Staa wa Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta amesema, Taifa Stars bado ina kazi kubwa ya kufanya ili kwenda Cameroon mwakani kwa ajili ya kushiriki mashindano ya AFCON.
Samatta ambaye alikuwa nchini kwa ajili ya Taifa Stars ilipokipiga na Cape Verde mechi ya kuwania kufudhu fainali hizo na ambapo walifungwa ugenini mabal 3-0 na kushinda nyumbano 2-0.
Amesema, mechi mbili walizobakiwa nazo dhidi ya Uganda 'The Cranes' na Lesotho wanatakiwa wapate matokeo mazuri ndipo wajiachie.
"Tumefanikiwa lakini safari bado ndefu. Ni kweli tumefanya vizuri mechi ya marudiano na Cape Verde hatutakiwi kubweteka,"alisema Samatta ambaye katika mchezo huo alikosa penalti lakini baadaye alitengeneza pasi ya mwisho ya bao lililofungwa na Simon Msuva sambamba na kufunga la pili.
Amesema, kinachotakiwa sasa ni mipango mizuri kwa ajili ya mchezo huo wa marudiano.
Akizungumzia penalti aliyokosa, Samatta amesema haikumsumbua kwa sababu alijua ana muda wa kufanya vizuri zaidi ndani ya dakika zilizokuwa zimebaki na akafanya kweli.
"Kwa sasa nimekuwa tofauti na ilivyokuwa zamani, nazijua changamoto hizi linisumbua kama dakika tano za mwanzo lakini baadaye nikakaa sawa,"alifafanua Samatta.
Kwa sasa Stars imefikisha pointi tano na ipo nafasi ya pili kwenye Kundi L nyuma ya Uganda wenye pointi saba, Cape Verde ya tatu wana nne na Lesotho wa nne wana mbili.