Dortmund yasaka mbadala wa Sancho

Munich, Ujerumani. HAKUNA anayejua nini kitatokea, lakini mabosi wa Borussia Dortmund wameanza kusaka mbadala wa winga wao, Jadon Sancho ambaye anahusishwa na kwenda Manchester United.

Sancho, 20, amekuwa akiwindwa muda mrefu na Man United ya Ole Gunnar Solskjaer na hatua ya Dortmund kusaka mbadala wake ni ishara kwamba, winga huyo wa Kiingereza yuko kwenye mlango wa kutokea.

Hata hivyo, kumekuwa na mjadala mzito kuhusu thamani ya Sancho, ambapo Dortmund wanataka kulipwa dau la pauni 100 milioni ili kuachia huku Man United wakitangaza kwamba, wako tayari kulipa pauni 50 milioni tu.

Mara kadhaa Dortmund wameonya kwamba, hawako tayari kukaa mezani kujadili ofa ya Sancho ambayo itakuwa chini ya pauni 100 milioni.

Hata hivyo, wameamua kujiandaa na maisha bila Sancho kwa kusaka winga mbadala kuendeleza makali katika kupambana na Bayern Munich kuwania mataji huko Bundesliga.

Mkurugenzi wa Ufundi wa Dortmund, Michael Zorc aliliambia Kicker kwamba: “Kama Sacho ataondoka, tunapaswa kufanya kitu kwa haraka kuziba nafasi yake. Tayari, kuna wachezaji wawili ambao tunawangalia kwa karibu maendeleo yao.”

Hata hivyo, Dortmund wanataka kuona Sancho akiendelea kukipiga klabuni hapo kwa msimu mmoja zaidi ili kuja kumuuza kwa bei kubwa tofauti na ilivyo sasa ambapo, klabu nyingi zimetikiswa kiuchumi kwa sababu ya janga la corona.