Dilunga, Ndemla, Mzamiru picha limeisha

Friday May 22 2020

 

By MWANDISHI WETU

TAARIFA njema kwa mashabiki wa Simba ni kwamba kabla ya Swala ya Al’asir kesho watakuwa na furaha ya kutosha.

Mastaa wao, Shiza Kichuya, Muzamiru Yasin, Said Ndemla na Hassan Dilunga wamejifunga tena Msimbazi kwa miaka miwili kila mmoja na kesho watatangazwa.

Awali Simba walisema kabla ya kuanza kusajili nyota wapya basi watahakikisha wamewaongezea mikataba wale wote wanaotaka kuendelea nao msimu ujao wa Ligi Kuu Bara.

Usajili mpya unaotajwa zaidi Simba ni wa beki Bakari Mwamnyeto anayeichezea timu ya Coastal Union ya jijini Tanga wakiwemo nyota wa kigeni.

Habari ambazo Mwanaspoti imejiridhisha nazo ni kwamba ishu ya Dilunga, Kichuya, Ndemla na Mzamiru imekwisha na sasa akili za viongozi zimehamia kwenye Ligi kwanza kutetea kombe lao.

Ingawa kocha wa Yanga, Luc Eymael amekuwa akisisitiza kwamba hakuna jina la Ndemla wala hamfikirii kwenye usajili wake, mchezaji huyo amekuwa akihusishwa na Yanga huku ikidaiwa kwamba ni dili iliyokuwa inachezwa na watu wake wa karibu ili kuwatia ubaridi Simba.

Advertisement

Habari zinasema kwamba Simba imewaongezea miaka miwili kwa masharti ya kuipandisha viwango vyao tofauti na mwenendo wao wa hivi karibuni.

Msimamo wa Simba ni kwamba wachezaji wote walioko kwenye vigezo vyote wanavyovitaka ikiwamo umri mdogo, ubora stahiki na afya njema, watapata mikataba ya miaka mitatu kila mmoja ili wakae muda mrefu klabuni na hata wakiuzwa Simba ifaidike.

Kuhusiana na usajili wa mastaa hao, Senzo Mazingisa ambaye ni Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, amesema hilo bado lipo mezani kwake kwa maana ya kwamba wanaendelea na mazungumzo lakini kesho Jumamosi kila kitu kitakuwa wazi.

“Kila kitu kilisimama kwasababu ya corona ingawa kuna mambo yalikuwa yanaendelea kwa umakini mkubwa ikiwemo kuzungumza na wachezaji ambao mikataba yao inaelekea ukingoni.

“Siwezi kuliweka hilo moja kwa moja kwamba tumemalizana na nyota hao zaidi tutalizungumzia hilo Jumamosi,” alisema Senzo ambaye hakutaka kukubali ama kukataa.

Simba walimsajili Kichuya wakati wa usajili wa dirisha dogo msimu huu akitokea ENPP ya Misri wakati wengine Ndemla na Mzamiru wapo Simba kwa zaidi ya miaka miwili huku Dilunga ndo anamalizika mkataba wake wa miaka miwili tangu achukuliwe kutokea Mtibwa Sugar.

Advertisement