Diamond kutoa ufadhili wa masomo

Muktasari:

 Mwanamuziki Diamond Plutnumz ametoa udhamini wa mwanafunzi mmoja wa shule ya Sekondari Rugambwa kwa atakayefanya vizuri katika masomo

HUENDA kiwango cha ushindani wa masomo kwa wanafunzi wa kidato cha nne kwa mwaka 2019 katika shule ya sekondari ya Rugambwa kikaongezeka maradufu baada ya mwanamuzi wa Bongo Flava, Naseeb Abdul 'Diamond Platnumz' na timu yake ya Wasafi Festival kufanya ziara katika shule hiyo.
Katika ziara hiyo, Diamond amejikuta akitangaza ufadhili wa masomo Marekani au Uingereza kwa mwanafunzi mmoja atakayefaulu kiwango cha juu katika masomo ya mtihani wake wa mwisho wa kidato cha nne.
Kuhusu utaratibu wa kuanza utekelezaji wa ofa hiyo, Diamond amesema atazungumza na uongozi wa shule kwa ajili ya kufanikisha ahadi yake.
Baada ya mazungumzo na uongozi wa shule, Diamond pia atazungumza na wadhamini wake katika tamasha la Wasafi ambao ni kwa ajili ya kupata nafasi moja ya ufadhili.
“Naamini hapa kila mtu ana kipaji tofauti na ili ufikie malengo lazima tusome kwa bidii katika masomo yetu,sasa kwakuwa mmenifurahisha  nitazungumza na waalimu wa hapa .
“Kwa mtu anayefanya vizuri katika masomo nitampa ufadhili wa kusoma Uingereza au Marekani na huu msaada ni nafasi ya kusoma chuo kwa mwanafunzi mmoja," alisema Diamond