Chidiebere: Popote kambi

Muktasari:

Pamoja na kuwa raia wa Nigeria, Chidiebere yupo nchini ambako inatajwa kuwepo familia yake, akitokea Zambia alikokuwa akiichezea Caps United ya Ligi Kuu nchini humo.

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Stand United, Chidiebere Abasirim  ni kama  amejiweka sokoni kwa kusema yupo tayari kujiunga na klabu yoyote msimu ujao wa Ligi Kuu Bara atakayofikiana nayo makubaliano.
Pamoja na kuwa raia wa Nigeria, Chidiebere yupo nchini ambako inatajwa kuwepo familia yake, akitokea Zambia alikokuwa akiichezea Caps United ya Ligi Kuu nchini humo.
Chidiebere anasema anajivunia kucheza soka la Tanzania hivyo kuwepo kwake nchini hakutamfanya aanze moja kuendana na kashikashi za Ligi hiyo ambayo imetoa wachezaji 20 watakaocheza fainali za mataifa ya Afrika nchini Misri.
“Nipo tayari kujiunga na timu yoyote kwa sababu mkataba wangu wa kuichezea Caps United umemalizika na sina mpango wa kurudi Zambia, mpira wa Tanzania umekuwa ukikua kwa kasi.
"Kuna timu zilizoonyesha nia ya kunihitaji lakini naangalia wapi ambako kutakuwa bora zaidi kwangu, naweza kufanya maamuzi ndani ya wiki mbili hadi tatu zijazo," alisema straika huyo.
Miongoni mwa timu ambazo zinahusishwa na mshambuliaji huyo mwenye nguvu  na uwezo wa kufunga mabao ya vichwa  ni timu yake ya zamani, Stand United iliyoshuka daraja,  Mwadui ya Shinyanga pamoja na Alliance ya Mwanza.