Chama aibukia Usajili Yanga

HUKO mtaani mashabiki wa Yanga wanacheka sana baada ya kusikia watani wao Simba wamemsajili Mbrazili na kiungo kutoka Sudan, Shiboub Sharaf Eldin.

Kinachowafanya waangushe kicheko ni baada ya kuangalia rekodi za nyota hao wapya wa kigeni wa Simba na kugundua hawatishi kama waliotua Jangwani.

Hata hivyo, kumbe kiungo Clatous Chama amewasikia na kuwatikisa mapema Jangwani kwa kuwaambia kwa jeshi linalosukwa Msimbazi, wasipojipanga watateseka sana.

Mzambia huyo aliyebakishwa kikosini kwa msimu ujao wa Ligi Kuu sambamba na Meddie Kagere na Pascal Wawa, amesema kwa namna timu yao inavyosukwa kwa msimu ujao haoni cha kuwazuia kuizima Yanga. Chama alisema sio kuizima Yanga tu, lakini pia anaamini Simba itatikisa michuano ya Afrika kuliko hata ilivyofanya msimu uliopita walipofika robo fainali ya Ligi ya Mabingwa.

Akizungumza na Mwanaspoti akiwa kwao Zambia, Chama alisema amekuwa akifuatilia kila kitu kinachoendelea nchini na hasa klabu yake na kufurahishwa na vifaa vilivyoshushwa Msimbazi.

Chama alisema kwa namna mabosi wao wanavyokiboresha kikosi chao cha msimu uliopita wakiingiza majembe mapya anaamini Simba itasumbua tena msimu ujao dhidi ya wapinzani wakiwamo Yanga.

“Ninayo furaha kuwa sehemu ya kikosi cha Simba msimu uliopita na natarajia hata msimu ujao nitakuwapo lakini kinachovutia ni namna kikosi kinavyoboreshwa.”

“Kwa sasa nipo mapumzikoni, lakini nafuatilia kila kitu na ninaamini maboresho yanayofanyika Simba yataifanya iwe tishio zaidi kuliko msimu uliopita na huenda tukatetea tena taji na kutikisa Afrika,” alisema Chama.

Kuhusu kinachofanywa na wapinzani wao Yanga kwenye usajili, Chama alisema wala hana hofu kwa sababu anajua timu yao imeanza kujipanga mapema.

“Usajili huo wa wenzetu unaweza kuleta changamoto, lakini bado Simba tupo vizuri zaidi kwani maboresho yanayofanywa yanaenda kuziba mapungufu ya msimu uliopita ambao tulitikisa Tanzania na Afrika kwa ujumla.”

Mpaka sasa Simba imeshasajili nyota wanne wapya wakiwamo wawili wa kigeni ambao ni straika Wilker Henrique Da Silva kutoka Brazili na Msudan Shiboub Sharaf Eldin ambaye ni kiungo mshambuliaji.

Wengine ni kipa Beno Kakolanya na mshambuliaji Miraj Athuman walikuwa Yanga na Lipuli, huku nyota wao wa zamani aliyekuwa Yanga, Ibrahim Ajibu akitajwa naye keshasaini mkataba wa miaka miwili.

NYOTA WAZIDI KUMIMINIKA

Katika hatua nyingine, Simba inaendelea kupokea nyota kadhaa wa kigeni wanaosaka nafasi ya kusajili Msimbazi na mabosi wa klabu hiyo wamewafungukia.

Imeelezwa nyota kibao wa kigeni wamekuwa wakitua nchini kwa ajili ya mazungumzo ya usajili na Simba lakini walio wengi wameshindwa kumalizana kutokana na aina ya uchezaji wao na mahitaji ya timu. Mmoja wa viongozi wa Simba (jina tunalo) alisema mpaka sasa kuna zaidi ya nyota 50 wametua kuomba kazi, lakini wanaendelea kuwafanyiwa tathmini na wataalamu waliowapa kazi kabla ya kuwasainisha.

Simba imebakiwa na nafasi zisizozidi tatu kwa nyota wa kigeni baada ya kuwasajili kina Sharaf Eldin na Da Silva, kwani inataka kuwa na wageni wasiozidi sana kwa sasa. Nyota hao saba ni pamoja na Kagere, Chama na Wawa waliobakishwa kikosini, ili nafasi zitakazokuwepo zije kujazwa kwenye dirisha dogo pale panapohitajika.

“Tuna kampuni yetu ya kuwachunguza na kuwatathimini wachezaji, ipo nje, hivyo kila mchezaji anayetakiwa Simba, lazima apitishwe huko kama anafaa ndipo sisi tunawapa mkataba,” alisema kiongozi huyo.

Mwenyekiti wa klabu hiyo, Swedy Mkwabi alipoulizwa juu ya taarifa hiyo alijibu; “Tunaendelea na usajili lakini mambo yetu tunayafanya kisasa zaidi, kila usajili watautangaza unapokamilika.”

“Kuna kikao cha mwisho cha Bodi kitakachojadili juu ya usajili kuona kwamba mahitaji yote aliyoyahitaji kocha wametimizwa ama lah, kama tutaona kuna sehemu inahitaji usajili basi tutafanya hivyo endapo hakutakuwepo na ulazima huo basi tutafunga na kuanza maandalizi ya msimu ujao,” alisema Mkwabi.