Cannavaro- Chalenji iwape ulaji vijana

Muktasari:

Wakati mashindano ya Chalenji yakiendelea nchini Uganda, beki wa zamani wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' amewataka wachezazi wa  Tanzania kutumia fursa ya kuonyesha uwezo wao ili wapate ulaji nje ya nchi.

Beki wa zamani wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' amesema mashindano ya Chalenji  yanayoendelea nchini Uganda ni fursa kwa wachezaji wa Tanzania kuonyesha uwezo wao.

Amesema kwenye soka kuna fursa nyingi za kuwasaidia wachezaji kufikia mafanikio ya kucheza soka  la kulipwa nje ya nchi, hivyo amewashauri ni wakati sahihi kwao kuonyesha maajabu kwenye mashindano hayo.

"Nimecheza katika mashindano hayo hivyo ninachokizungumza namaanisha na  najua watafaidika wale ambao wataamua kuona fursa hiyo, wakijituma ni faida kwa timu za taifa  na  kwao pia ,"

"Kwenye mashindano kama hayo kunakuwa na watu wa aina tofauti mfano mawakala pamoja na viongozi wa timu wanazocheza nazo hivyo wajitume ili waweze  kuonwa na kufika mbali,"amesema Canavaro.

Cannavaro amesema  timu za Tanzania zina vijana wenye vipaji  ambavyo  vina nafasi kubwa ya kuwashangaza wadau wanaofuatilia mashindao hayo.

Kilimanjaro Stars  inatarajia kucheza na Sudan kesho Jumamosi na endapo itashinda itatinga nusu fainali.