Bodi ya Filamu yakunwa na kiwango cha Sinema SZIFF

Muktasari:

Sinema hizo zimeanza kuonyeshwa mwishoni mwa wiki  katika ukumbi wa sinema wa City Mall, uliopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam huku  Red Flag iliyochezwa na msanii wa kitanzania Rammy Galis na The Cut ya nchini Kenya zikifungua dimba.

Katibu Mtendaji wa bodi ya filamu, Joyce Fisoo,  amekoshwa na kiwango, zitakazoshindanishwa katika  tuzo za Sinema Zetu International Film Festival(SZIFF), Februari mwaka huu.
Sinema hizo zimeanza kuonyeshwa mwishoni mwa wiki  katika ukumbi wa sinema wa City Mall, uliopo katikati ya Jiji la Dar es Salaam huku  Red Flag iliyochezwa na msanii wa kitanzania Rammy Galis na The Cut ya nchini Kenya zikifungua dimba.
Akizungumza mara baada ya kutoka kutazama filamu hizo, Fisoo, amepongeza uchaguzi wa waliohusika kuchagua sinema hizo kupeleka katika ukumbi wa sinema ambapo alidai kazi zinazoonyeshwa huko huwa ni za kiwango cha juu.
Kutokana na hilo, Katibu huyo amewasihi wasanii na watayarishaji filamu kujitokeza kwa wingi katika siku zilizobaki kwenda kujifunza wenzao wanafanya nini katika tasnia hiyo ili kuweza kuboresha kazi zao.
"Kama mnavyojua sinema hizo zitakuwa kutoka nchi mbalimbali, ni wakati wa wasanii wetu kujitokeza kujifunza kwani baadhi ya nchi zimeaza kufanya kazi hiyo muda mrefu na zina vifaa vya kisasa hivyo ni vema watu wakaenda kuchota ujuzi na kuwea kuboresha kazi wanazotarajia kuzitengeneza siku za mbele" amesema.
Naye Mkurugenzi wa  vipindi wa Azam ambaye ndio waandaaji wa tuzo hizo, Yahaya Mohamed, amesema sinema hizo zitaonyeshwa kila siku hadi Februari 10 mwaka huu,ambapo majaji watachagua zilizo bora.
Kwa upande wao baadhi ya wasanii akwemo Rammy Galis, amesema utaratibu ulioletwa na Azam kupeleka filamu zao kwenye majumba ya sinema utaipaisha tasnia ya filamu hapa nchini mbali.
Wakati Chuchu Hans amesema ni wakati sasa wasanii kufanyia kazi malalamiko waliyoyapokea kuhusu ubora wa filamu zao kwa muda mrefu kwa kuwa sasa wanaenda katika soko jingine.
Mwaka huu katika tuzo hizo ambazo ni mara yake ya pili kufanyika, Azam imeshindanisha filamu na sinema ambapo filamu zitapigiwa kura na watazamaji wa chaneli ya Sinema zetu huku sinema zikichaguliwa na majaji