Bigirimana amchomoa Boxer kwa Zesco

WINGA wa Yanga Mrundi, Issa Bigirimana amerejea kikosini na atakuwa miongoni mwa nyota watakaoondoka keshokutwa Jumatau kuelekea Zambia kuvaana na Zesco katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Juzi Alhamisi, Bigirimana alionekana kwenye mazoezi na wenzake yaliyofanyika uwanja wa Chuo cha Polisi Kurasini na Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela alisema kikosi chao kitaondoka na nchini na kuweka kambi Lusaka huku kikiendelea kumkosa beki wao wa kulia Paul Godfrey ‘Boxer’ ambaye hata mchezo wa kwanza hakuwepo.

Mwakalebela alisema kuhusu Bigirimana anaendelea vizuri na kwa ripoti iliyopo ni kwmaba yupo fiti kuiwakilisha timu hiyo yao kwenye mchezo huo utakaochezwa uwanja wa Levy Mwanawasa mjini Ndola.

“Maandalizi yote ya timu siku ya kuondoka mpaka ambapo itafikia na kucheza mechi ya marudiano yanakwenda sawa kilichobaki ni benchi la ufundi kutangaza wachezaji wanaowahitaji ili kutuwakilisha huko,” alisema Mwakalebela.

Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli alisema wataondoka na orodha kamili ya wachezaji na viongozi ambao watatangazwa rasmi leo Jumamosi.

“Bigirimana tutakuwa naye kwani tangu amerudi ameonekana kuwa fiti ambapo tutamkosa Boxer ambaye hayupo fiti na bado anaendelea kuuguza maumivu hivyo ataukosa mchezo huu,” alisema Bumbuli.

Kukosekana kwa Boxer kutamfanya Kocha Mwinyi Zahera amtumie Mapinduzi Balama mwenye uwezo wa kucheza beki ya kulia ingawa kiasilia ni kiungo mshambuliaji kama ilivyokuwa mechi ya kwanza au Ali Ali na Mustapha Selemani ambao kiasilia ni mabeki wa kati.

Katika mchezo wa kwanza uliochezwa uwanja wa Taifa, Yanga walilazimishwa sare ya bao 1-1 ambapo Yanga walipata bao kwa mkwaju wa penalti kupitia Patrick Sibomana kisha, Thabani Kamusoko kusawazisha dakika za lala salama.

Yanga inahitaji ushindi ama sare ya mabao kuanzia mawili kwenye mechi yao itakayopigwa mwishoni mwa wiki ijayo baada ya sare hiyo ya uwanja wa nyumbani na kama itapenya Ndola, itafuzu makundi na kama itatokea bahati mbaya itaangukia kwenye mchujo wa mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika.