JICHO LA MWEWE: Bernard Morisson na James Kotei wanatoka taifa moja?

NILIKWENDA Accra mwaka 2008 kwa ajili ya kushuhudia michuano ya Afcon. Kuna jambo lilinishangaza kidogo. Mechi fulani hivi ya Ghana alikuja Rais wa zamani wa nchi hiyo, Jerry Rawlings. Jamaa ni mwanajeshi mzuri tu.

Kilichonishangaza ni jinsi alivyokuja uwanjani na kukaa katika jukwaa la kawaida kabisa la mashabiki. Yaani ni kama vile Rais mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete afike Uwanja wa Taifa na kuamua kukaa upande wa jukwaa la Mashariki.

Kilichonishangaza zaidi kwa Rawlings ni hakuwa na walinzi wengi. Kama si wawili basi walikuwepo watatu. Alikaa kwa amani mpaka alipoondoka. Nikajiuliza. Ni kiburi? Jeuri? Au anapendwa sana na wananchi wake? Sikuwahi kuelewa.

Ndani ya nchi yenyewe, Waghana ni watu wenye upendo sana. Zamani nilikuwa nawalinganisha sana na Wanigeria kumbe nilikosea. Niliwakuta Waghana wakiwa ni watu wenye upendo mwingi na wasiokuwa na makuu. Niliondoka Ghana na taswira hiyo.

Wasiwasi wangu na Waghana ulianza miaka miwili baadaye. Nilikwenda Mwanza kushuhudia pambano kati ya Simba na Yanga lililochezwa katika Uwanja wa CCM Kirumba. Baada ya mechi kuna siri kubwa ambayo nilikuja kuambiwa.

Niliambiwa kipa wa Yanga, Yaw Berko, ambaye ni raia wa Ghana alikuwa amegoma kucheza mechi hiyo kwa madai alikuwa hajisikii vizuri kabisa. Viongozi wa Yanga walishinda katika mlango wa chumba cha Berko wakimsihi acheze.

Berko alikuwa anadengua tu. Baadhi ya mabosi wa Yanga waliamua kuchanga na kumpatia Dola 300 ili acheze mechi hiyo. Mabosi wa Yanga hawakumwamini kabisa, Ivan Knezevic ambaye wakati Berko anadengua yeye alikuwa akipasha misuli yake moto katika korido ya hoteli akijigamba alikuwa tayari kucheza mechi hiyo.

Hatimaye Yanga walifanikiwa kumshawishi Berko na akadaka vyema katika pambano hilo akiokoa michomo ya washambuliaji wa Simba.

Yanga walishinda 1-0 shukrani kwa bao maridadi la Jerson Tegete ambaye alimfunga vyema Juma Kaseja baada ya kubaki naye ana kwa ana langoni.

Kuanzia hapo nilianza kupata wasiwasi kuhusu Berko. Akaanza kunipa wasiwasi kuhusu tabia za Waghana. Hata hivyo, sikumhukumu sana. Huenda ilikuwa tabia yake binafsi, ingawa waswahili zamani walikuwa na msemo wao ‘Samaki mmoja akioza wote huoza’.

Majuzi tena kuna Mghana mwingine alinishangaza sana. Lamine Moro. Lile teke ambalo alimpiga Mwinyi Kazimoto katika pambano la Yanga na JKT Tanzania liliniachia maswali mengi. Hata wachezaji wetu masela kama kina Juma Nyosso wameacha kufanya matukio yale ya ajabu.

Kwa jinsi nilivyowaona Waghana mwaka 2008 pale kwao sikuamini kama tungeweza kuwa na mchezaji wa aina ya Lamine. Kwa nini alifanya vile? Alitoka alikotoka umbali wa hatua 30 na bado hakuweza kuhimili hasira zake kwenda kuendeleza vurugu katika pambano lile dhidi ya JKT Tanzania pale Dodoma.

Achana na Lamine. Sasa tuna Mghana mwingine ambaye anafanya matukio nje ya uwanja. Bernard Morisson. Huyu kazua kichekesho majuzi. Taarifa za uhakika ambazo ninazo ni amesaini mkataba wa miwili na Yanga Machi mwaka huu.

Kimazingira tu ungeweza kuamini Morisson amesaini Yanga. Matajiri wa GSM wangeruhusu vipi mchezaji huyu aliyejenga jina Yanga, akawafunga pia Simba kwa juhudi binafsi, afike mpaka mwishoni mwa msimu bila ya kusaini mkataba mpya?

Amekwenda na mkataba wake TFF akitaka aruhusiwe kuwa huru. Je Yanga wamefoji mkataba wake? Achana na hilo.

Usiku mmoja kabla ya pambano kati ya Yanga na Kagera Sugar alilazimisha kuondoka kambini usiku.

Alizuiwa na meneja wa klabu, lakini akaamua kuchukua kisu na kutishia kumchoma yeyote ambaye angemzuia.

Hatimaye alifanikiwa kuondoka zake na baadaye kutaka kurudi. Yanga walimwondoa katika kambi na wakafanikiwa kushinda mechi yao.

Wakati ukidhani ugomvi wa Yanga na Morisson ungewasambaratisha kumbe ndio kwamba sinema ilikuwa inaanza. Majuzi tukamuona Morisson akiwa katika kambi ya Yanga. Akiwa amejawa na furaha. Ameshasahau kilichotokea. Nikajiuliza,

“Huyu jamaa ana akili zake timamu kweli?”

Zile picha ambazo Yanga wamezisambaza wote tukazishangaa. Kesho yake akaibuka tena mazoezini. Katushangaza sana. Ana akili timamu? Nikajiuliza. Nilidhani huo ulikuwa mwanzo wa bifu nzito kati yake na klabu kiasi asingejali kwenda mazoezini. Kwa nini aende mazoezini katika klabu ambayo ‘imefoji’ mkataba wake?

Baada ya tukio lile ndio nikaanza kujumlisha matukio kutoka kwa watu wa Ghana. Kumbe inaweza kuna kitu hakipo sawa katika vichwa vyao? Tatizo bado naendelea kuwafikiria hasa nilipokutana na ukarimu wa watu wa Ghana mwaka 2008 pale Accra.

Si watu wa Ghana tu, hapa hapa nchini kuna mastaa kibao wa Ghana wamewahi kuja. Hawakuwa na akili za Jerry Rawlings, Yaw Berko, Lamine Moro wala Morisson.

Mfikirie James Kotei jinsi alivyokuwa mtu muungwana. Inafikia wakati unajiuliza, hivi Kotei na Morisson wanatoka taifa moja?