Beki Van Dijk aongezea majeruhi Liverpool

Muktasari:

Kuumia kwa beki Virgil van Dijk na mshambuliaji Mo Salah, wakati wakizitumikia timu zao za Taifa, kumempa hofu kocha Jurgen Klopp wa Liverpool katika harakati zake za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu England.

Amsterdam, Uholanzi. Nahodha wa Uholanzi, Virgil van Dijk ameongezea idadi ya majeruhi ndani ya kikosi cha Liverpool.

Mchezaji huyo alijitonesha akiwa katika majukumu ya Taifa ambapo timu hiyo inajiandaa kwa mchezo wa kirafiki wa ugenini dhidi ya Ubelgiji utakaopigwa kesho.

Mlinzi huyo amesafirishwa kurejea Liverpool wakati wenzake wakielekea Ubelgiji na ataungana na majeruhi mwingine mpya Mohamed ‘Mo’ Salah aliyeumia juzi wakati akiitumkia Misri katika mechi ya kufuzu fainali ya Afrika.

Majeruhi wa muda mrefu ndani ya timu hiyo ni pamoja na mshambuliaji Alex Oxlade-Chamberlain, kinda Divock Origi na Rhian Brewster, huku James Milner na Adam Lallana wakitarajiwa kurejea hivi karibuni.

Mo Salah aliifungia Misri bao wakiichapa Swatini zamani Swaziland mabao 4-1, wakati Van Dijk aliumia katika mchezo alioifungia Uholanzi bao katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Ujerumani wa kufuzu ‘Nations Ligi’, kuumia kwao ni pigo kwa Kocha Jurgen Klopp.

“Van Dijk aliumia kwa mara ya kwanza katika mchezo dhidi ya Southampton na alianza kupona kabla ya kujitonesha akiitumikia timu ya Taifa hivyo atakosekana uwanjani kwa wiki mbili,” ilisema taarifa ya klabu.

Kocha wa Liverpool anatamani kutompoteza mchezaji yeyote katika mechi zake za sasa lakini amebainisha kuwa hatawatumia Van Dijk na Mo Salah katika mechi ya wikiendi hii ya ugenini dhidi ya Huddersfield.