Beki KMC anukia Ufaransa

IDADI ya nyota wa Kitanzania kutimka nje ya nchi kwenda kukipiga soka la kulipwa huenda ikaongezeka baada ya beki wa KMC, Ally Msengi, kujiandaa kutimka kwenda Ufaransa kutesti zali katika klabu ya Lille iliyopo Ligi Kuu ya nchini humo (Ligue 1).

Kampuni ya Siyavuma Sports Agency, inayomsimamia mchezaji huyo, ndiyo imefichua mpango huo ikiwa ni mikakati ya kuona nyota wa soka nchini wakiongezeka kwenye kucheza nje ya nchi.

Mratibu wa kampuni hiyo nchini, Michael Mwebe alisema wapo katika mipango ya kumpeleka Msengi KMC kwenye majaribio katika klabu ya Lille.

“Mipango ikikaa vyema Msengi ataenda kufanya majaribio Ufaransa, kila kitu kinaendelea sawa kwa sasa,” alisema Mwebe na kuongeza;

“Kwa hapa nyumbani kampuni hii ina wachezaji wachache inayowasimamia wengine tupo nao kwenye mazungumzo, ila wanaocheza Ligi Kuu ya ndani ni Ally Msengi (KMC), Shaaban Adda (Lipuli) na Mohammed Rashid (Singida Utd),” alisema.