Bayern Munich yakoroga mambo kuhusu Sane

Munich, Ujerumani. Mabingwa wa Ligi Kuu Ujerumani (Bundesliga), Bayern Munich wameiomba radhi Manchester City baada ya kuchapisha picha ya winga Leroy Sane ikimuonyesha akisaini kujiunga nao na nyingine akiwa na jezi za miamba hiyo ya Allianz Arena kabla ya usajili rasmi kutangazwa.

Winga huyo Mjerumani ameripotiwa kusaini mkataba wa miaka mitano kwenye kikosi cha Bayern Munich baada ya kunaswa akitokea Man City kwa Pauni 54.8 milioni.

Uhamisho huo haujatangazwa rasmi, ambapo ilidaiwa kwamba Sane alikuwa akisubiriwa akamilishe vipimo vya afya, lakini picha zilizotumwa kwenye mitandao ya kijamii zinamwonyesha akisaini mkataba huku ikielezwa ilichapishwa kwenye tovuti ya Bayern Munich ya lugha ya Kiarabu. Kwa mujibu wa Sky Sports, Bayern Munich wameripotiwa kuomba radhi kwa hilo.

Man City na Bayern Munich zimefikia makubaliano kuhusu ada ya Sane mapema wiki hii ambapo miamba hiyo ya Ujerumani itatanguliza kulipa Pauni 45 milioni na Pauni 9.8 milioni zitalipwa kutokana na mafanikio ya ndani ya uwanja ya mchezaji.